CHADEMA KATAVI WABARIKI KUNG'OREWA MWENYEKITI

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chadema mkoani Katavi wameridhia kwa kauli moja na kubariki uamuzi wa kumsimamisha uongozi Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama hicho, John Malack na viongozi wengine watatu waandamizi wa chama hicho, Jimbola Mpanda Mjini.

Viongozi hao watatu ni pamoja na Mwenyekiti wa chama hicho Jimbo la Mpanda Mjini, Seif Sipia, Katibu wa jimbo hilo, Joseph Mona ambaye pia ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini kwa tiketi ya chama hicho, Said Arfi.

Katika orodha hiyo yupo pia KatibuMwenezi wa chama hicho, Godfrey Maufi ambaye ameshavuliwa uanachama wa chama hicho akidaiwa kuiba nyaraka za siri za chama hicho na kuzisoma katika mkutano wa hadhara.

Pia mkutano huo umependekeza kuvuliwa uanachama wa chama hicho watu kadhaa akiwemo Iddi Nziguye ambaye ni Diwani kwa tiketi ya chama hicho Kata ya Makanyagio na Diwani wa Kata ya Kashaulili, John Matongo.

Uamuzi huo ulifikiwa juzi na wajumbe wa mkutano huo mkuu wa chama hicho uliofanyika mjini hapa ukiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema wa Kandaya Magharibi, Masanja Mussa Katambi.

Februari 22 mwaka huu kikao cha mashauriano cha chama hicho ngazi ya mkoa kiliwasimamisha viongozi hao, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho mkoani hapa, Malack akituhumiwa kufungua na kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Februari 2, mwaka huu ambao unadaiwa uliwakashifu viongozi wa chama hicho ngazi ya Taifa.