Beraniho (20) ambaye emepewa pia uraia wa England amesema kwamba hana nia ya kufungua mashitaka dhidi ya mchezaji mwenzake, James Morison aliyempiga na kwamba wawili hao walikutana, kuzungumza kidugu na kumaliza mambo.
Kocha Pepe Mel amesema anaamini kwamba kinda huyo atakuwa na msaada mkubwa katika mikakati ya klabu hiyo kuinusuru timu kushuka daraja msimu huu. West Brom walikuwa wakiongoza hadi dakika za majeruhi ambapo Beraniho alipokonywa mpira na kuzaa bao la Cardiff Jumamosi iliyopita.
Baada ya mechi hiyo lilizuka zogo kubwa hadi kwenye chumba cha kubadilishia nguo ambapo wachezaji kadhaa walimvaa Beraniho kwa madai kwamba alicheza kizembe. Hata hivyo, Beraniho ndiye aliifungia timu bao muhimu la ushindi dhidi ya Manchester United na pia bao muhimu dhidi ya Arsenal.
Beraniho alikuwa na uamuzi wa kufuatilia suala hilo kisheria ili apate haki yake na Morrison aadhibiwe kwa ngumi aliyomtwanga.
"Beraniho atakuwa muhimu sana kwetu katika mechi saba zinazokuja," akasema Mel na kuongeza kwamba hakuna hatua zozote za kinidhamu zilzochukuliwa kuhusiana na tukio hilo.
Msemaji wa klabu alisema kutokea zogo kama hilo ni kawaida baada ya mechi kwa klabu nyingi, na kwambahiyo inaonesha kwamba wachezaji wanajali na wasingependa kuona wanapoteza mechi.
"Wachezaji walimalizana wenyewe kama walivyolianzisha na sasa mambo yanaendelea vyema na kwa Beraniho na Morrison ni kana kwamba ni ndugu wa familia moja.
Nimezungumza na Beraniho na anaonesha kujali kuliko watu wengine wa umri wake mdogo.
Nimemweleza kwamba namwamini na kumtegemea kwa mafanikio ya timu yetu," akasema kocha huyo.
AARON RAMSEY AREJEA DIMBANI
Kiungo Aaron Ramsey aliyewabeba Arsenal tangu mwanzo wa msimu hadi alipoumia Desemba 26 mwakajana, anarejea uwanjani.
Ramsey (23) ni moja ya sababu za Arsenal kupanda hadi nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi, lakini mambo yalibadilika tangu kuumia kwake na wenzake wakiwamo Theo Walcott, Alex Oxlade-Chamberlain ambapo timu ilianza kuporomoka.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema nyota huyo ambaye msimu huu ameshafunga mabao 13 licha ya kuwa nje kwa mechi nyingi, atakuwa kwenye kikosi kinachosafiri kukabiliana na Everton kwenye dimba la Goodison Park Jumapili hii.
Mchezaji huyu wa Timu ya Taifa ya Wales alikuwa anasumbuliwa na nyonga, na aliumia wakati timu yake ikipata ushindi wa 3-1 dhidi yaWest Ham. Wenger amesema kuwa na mtu kama Ramsey anayeweza kuisaidia timu ni muhimu sana.
Arsenal sasa wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 64 huku Everton wakiwafuatia kwa pointi 60 na bado wana mchezo mmoja mkononi. Liverpool wanaongoza ligikwa pointi 71, Chelsea wana pointi 69 na Manchester City wanazo 67 na michezo miwili mkononi.
Nafasi ya sita inashikwa na Tottenham Hotspur ambao kama Everton wanagombea kuwapokonya Arsenal nafasi ya nne ili kuwa moja ya timu nne zitakazoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Spur wana pointi 56 hivyo bado wapo mbali.
BENTEKE NJE MIEZI SITA
Wakati Ramsey akirejea, Aston Villa wamepata pigo kubwa baada ya mpachika mabao wao, Christian Benteke kuumia mazoezini na imeelezwa kwamba hatacheza kwa miezi sita ijayo.
Benteke (23) aliumia kwenye mazoezi ya timu hiyo, na inamaanisha pia kwamba hataweza kuiwakilisha nchi yake ya Ubelgiji kwenye michuano ya Kombe la Dunia Brazil inayoanza Juni 12 mwaka huu.
Kocha wa Villa, Paul Lambert alisema habari hizo ni za kusikitisha sana kwa Benteke mwenyewe na klabu kwa sababu alihitaji na kuhitajiwa kucheza wakati huu kuliko mwingine wowote.
Benteke aliyezaliwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kabla ya kupata uraia wa Ubelgiji alijiunga na Villa Agosti 2012 kwa kitita cha pauni milioni saba akitoka klabu ya Genk ya Ubelgiji.
Msimu uliopita aliifungia timu yake mabao 23 kwenye mashindano yotelakini baadaye alitikisa kibiriti kuondoka kabla ya kupozwa na kukubali kubaki. Msimu huu amefunga mabao 11 tu na amekwenda miezi mine bila kufunga hata moja.