Habari kutoka ndani ya Umoja huo zinasema kuwa angalau viongozi wawili wa vyama vinavyounda UKAWA wanataka kurejea bungeni na kushiriki mchakato wa kutunga Katiba mpya wakati Bunge hilo litakapoanza tena Agosti mwaka huu.
Habari zinasema kuwa viongozi hao wawili, wanataka kurejea tena bungeni kwa sababu wameanza kubaini kuwa kuna ujanja mwingi ndani ya UKAWA na kuwa baadhi ya vyama vinavidanganya na kuvitumiavingine, bila kuonekana kwa faida yoyote dhahiri.
"Tulisusa Bunge kwa pamoja, lakini sasa inaanza kuonekana kuwa wapo wenzetu ambao wana maslahi binafsi na kuonekana kututumia sisikwa manufaa yao ya kisiasa na hata kifedha," anasema mmoja wa viongozi wa UKAWA, ambaye anahisi baadhi ya wenzao wanapata maslahi zaidi kuliko wengine.
Kuna madai kuwa UKAWA wamepatiwa fedha, tena nyingi na mfadhili ama wafadhili wa nje ya Tanzania, lakini fedha hizo zinaishia mifukoni mwa kiongozi mmoja amawawili wa umoja huo, usiosajiliwa na unaoendesha shughuli zake za kisiasa, bila hati zozote za kuuhalalisha kuendesha shughuli za kisiasa.
Viongozi wa vyama CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na vyama vingine vidogo vidogo walisusa Bunge Maalumu la Katiba mwezi uliopita, wakiazimia kuendesha kampeni ya kutafuta Katiba mpya nje ya Bunge, kupitia mikutano ya hadhara ya wananchi. UKAWA walifanya mkutano wao wa kwanza mjini Zanzibar juzi.
Pamoja na kwamba ni dhahiri kuwa Umoja huo na shughuli zake haziungwi mkono na wananchi wa Tanzania walio wengi, lakini viongozi wake wameendelea kushikilia kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima.
Wachunguzi wa masuala ya kisiasa, wanasema kuwa UKAWA wamechagua kuanzia mikutano yao Zanzibar, kwa sababu huko ndiko wana uhakika wa kupata watu wa kuhudhuria mikutano yao, kwa sababu ya wanachama wa CUF.
"Wamekimbia Zanzibar kwa sababu huko Bara watampata nani wa kwenda kupoteza muda wake kusikiliza hoja zisizokuwa na mashiko," amesema mchunguzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro.