WATALII TOKA UINGEREZA WATOROKA MOMBASA

Mamia ya watalii kutoka Uingereza waliokuwa kisiwani Mombasa Kenya wamelazimishwa kurejea makwao baada ya serikali ya nchi hiyo kutoa tahadhari ya tishio la mashambulizi ya kigaidi nchini Kenya.

Kampuni zinazopanga safari za watalii kutoka Uingereza Thomson na First Choice zilifutilia mbali safari zote zilizokuwa zimepangwa kuwaleta watalii Mjini Mombasa hadi mwezi Oktoba zikihofia usalama wao.


Gazeti la The Telegraph linasema kuwa takriban watalii 500 kutoka Uingereza wataathirika na kauli hiyo.

Tahadhari hiyo kutoka kwa serikali ya Uingereza imesema kuwa wanamgambo wa kiislamu kutoka nchi jirani ya Somalia al-Shabab huenda wakafanya mashambulizi nchini Kenya.

Ilani hiyo iliwaonya raiya wote wa Uingereza ambao wako nchini Kenya kwa shughuli ambazo si za dharura waondoke takriban kilomita 60 kutoka kwenye mpaka kati ya kenya na Somalia.

Kampuni ya utalii ya Thomson imewarejesha nyumbani kundi la kwanza la watalii huku waliosalia wakiratibiwa kuondoshwa ijumaa.

Watalii walishauriwa wasizuru kisiwa cha Mombasa huku wakishauriwa kuwa Diani beach na Uwanja wa ndege wa Moi Mombasa ni salama kwao.


Al Shabab

Al-Shabab imeimarisha mashambulizi katika eneo hilo katika siku za hivi punde kundi hilo likisisitiza kuwa linalipiza kisasi vitendo vya majeshi ya Kenya nchini Somalia.

Ilani hiyo ilionya kuwa kuna uwezekano mkubwa wa matukio ya ugaidi na utekaji nyara.

Huku wakionywa kuwa waepuke maeneo ya hadhara ambayo yamejaa watu.

Ndege zinazowarejesha nyumbani watalii hao zimekodishwa na serikali ya Uingereza.


Marekani ,Ufaransa na Australia pia zimeagiza raiya wao walioko pwani ya Kenya kuondoka mara moja.

Mtalii moja Augustine Conall ameiambia shirika la habari la Reuters kuwa jamaa na familia zao wamekuwa wakihofia usalama wao na kuwashauri kurejea Uingereza.


Mwengine Matilda Evanalisema kuwa hamini siku zake 6 za kujivinjari zimekatizwa na makataa hiyoya kuondoka Mombasa.

Mapema mwezi huu watu watatu waliuuawa katika mlipuko uliotokea katika kituocha mabasi ya umma mjini humo.


Mlipuko mwingine umetokea katika mtaa wa kifahari wa Nyali.

Miezi miwili iliyopita polisi mjini humo waliwakamata watu wawili waliokuwa wakiendesha gari lililokuwa limebeba mabomu mawili ya kujitengenezea yenye uwezo wa kubomoa jengo lenye gorofa Kumi.


Polisi walisema kuwa watu hao wawili - mmoja Mkenya na mwingine mwenye asili ya Kisomali - walikuwa wakilenga eneo fulani mjini mhumo.

Hata hivyo hali ya usalama nchini Kenya imekuwa katika hali ya tahadhari tangu kufanywe mashambulizi katika maduka ya Westgate Jijini Nairobi Septemba, mwaka uliopita, ambapo zaidiya watu 67 walifariki.


Kundi la wapiganaji wa Alshabab walidai kuhusika nawakaahidi kuendelea na mashambulizi nchini Kenya hadi pale majeshi ya Kenya itakapoondoka Somalia.

Mwezi februari zaidi ya watu 100 walifikishwa mahakamani mjini Mombasa na kushtakiwa kwa kuwa wanachama wa Al Shabaab baada ya maafisa wa usalama kufanya operesheni katika msikiti mmoja hapo mjini mombasa.