WASICHANA WENGINE 8 WATEKWA NIGERIA

Washukiwa wa kundi la wapiganaji wa kiisilamu nchini Nigeria, Boko Haram, wamewateka nyara wasichana wengine 8 Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.


Tukio hili la hivi karibuni la utekaji nyara, lilifanyika Jumapili, katika kijiji cha Warabe katika jimbo la Borno.

Wasichana waliotekwa nyara wako kati ya umri wa miaka 12 na 15.

Mnamo siku ya Jumatatu, kiongozi wa kundi hilo alitishia kuwauza wanafunzi 230 waliotekwa nyara na kundi hilo katika shule ya Chibok tarehe 14 mwezi Aprili.

Kundi la Boko Haram limewaua maelfu tangu mwaka 2009. Lengo lake kuu ni kupinga elimu ya kimagharibi na kutaka utawala wa kiisilamu.

Kwa mujibu wa mhariri wa idhaa ya Hausa Mansur Liman, eneo la Warabe ambako wasichana wanane walitekwa nyara, ni ngome yakundi hilo la kiisilamu.

Wapiganaji waliwasili katika lori mbili huku wakiiba chakula na mifugo kutoka katika kijiji hicho.


Kuna tatizo la mawasiliano katika kijiji hicho sababu kuu ya kuchelewa kutolewa kwa taarifa hizo za utekaji nyara.


Waandamanaji wamekuwa wakifanya maandamano kuishinikiza serikali kuharakisha juhudi zake za kuwaokoa wasichana waliotekwa nyara tarehe 14 Aprili.

Kijiji hicho pia kiko akribu na msitu Sambisa ambako kikundi cha kwanza cha wanafunzi waliotekwa nyara walipelekwa.


Kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau, alitoa kanda ya video siku ya Jumatatu kudai kuwa kundi hilndilo liliwateka nyara wanafunzi hao na kwamba linapanga kuwauza.