Akizungumza juzi wakati wa kufunga semina ya viongozi wa diniwa Mkoa wa Kilimanjaro iliyofanyika katika ukumbi wa Umoja Hostel, Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji nchini, Askofu Ikongo alisema kauli za Askofu Kakobe zimekuwa za hatari na zinaweza kuliingiza Taifa kwenye machafuko ya kidini.
"Nchi yetu imekuwa na dalili za viashiria vya kutoweka kwa amani na utulivu, kutokana na baadhi ya viongozi wa dini kujiingiza kwenye siasa na kuanza kutoa kauli za kuashiria uchochezi na kupandikizachuki kwa waumini…sasa umefika wakati sisi viongozi wa dini hatuwezi kunyamaza kwani tutaonekana na matamko yanayotolewa kiholela kwa kutumia mwamvuli wa upentekoste," alisema Askofu Ikongo.
Alisema Askofu Kakobe amekiuka uadilifu wake, kwani Aprili 20 mwaka huu katika kanisa lake la Mwenge, alitoa kauli kuwa atapambana hadi Tanganyika irudi hata kwa kukatwa kichwa, kauli ambayo inadhihirisha ugaidi.
Askofu Ikongo alisema kauli kama hiyo haistahili kutolewa na mtumishi yeyote wa Mungu, kwanimtu mwenye uwezo wa kusema hata akatwe kichwa sio wa kawaida bali ni mtu aliye na mafunzo ya kujitoa mhanga kama gaidi.
"Tunasikitishwa na kauli za Askofu Kakobe ambazo zinaweza kuliletea Taifa machafuko ya kidini…siku ya Pasaka Aprili 20 mwaka huu aligeuza mimbari kuwa jukwaa la siasa, kwa kuhubiri uchochezi kwa kudai; kila mtu anayepigania kurudi kwa Tanganyika, ana Mungu ndani yake," alisema.
Kwa mujibu wa Askofu Ikongo, kauli hizo za Kakobe ni za kigaidi na zina nia ya kuvuruga amani ya Watanzania na kuliingiza taifa kwenye machafuko, ambayo yataharibu tunu iliyoachwa na Babawa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema ni vyema viongozi wa dini wajikumbushe wajibu wao wa kuliombea Taifa, na kuwaongoza waumini wao kufuata yaliyo mema badala ya kugeuka sehemu ya kutumiwa na wanasiasa.
Akifunga semina hiyo Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Makiluli aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Leonidas Gama, alisema inasikitisha kuona viongozi wa dini kutumiwa na wanasiasa, kwa kutoa kauli zinazowafanya wananchi kuhoji kama viongozi hao hawatumii dini kutekeleza malengo ambayo sio mema.
Alisema Serikali bado ina imani na viongozi wa dini, kwa wale wanaozingatia maadili na utume wao wa kuhakikisha amani iliyodumu kwa miaka mingi inadumishwa.
Aliwataka waumini kutowaunga mkono wanaotumia mimbari kuwa jukwaa la siasa kwa kutoa maneno makali yanayohatarisha amani na kupandikiza chuki miongoni mwa waumini na wananchi.