WATU WAWILI WAJERUHIWA KATIKA MLIPUKO WA BOMU

Watu wawili wamejeruhiwa katika mlipuko uliotokea mjini Mombasa pwani ya Kenya.

Miongoni mwa wawili hao ni afisa wa polisi aliyekimbizwa katika hospitali ya mkoa kupokea matibabu.

Shambulio hilo lilitokea wakati maafisa wa polisi walimkamata mshukiwa wa ugaidi, na hapo pakatokea mtu wa pili aliyewarushia guruneti katika jitihada ya kumuokoa mshukiwa aliyekamatwa.

Mbunge wa Mvita kutoka eneo hilo, Abdulswamad Sharrif ambaye ni miongoni mwa viongozi waliofika katikaeneo hilo punde baada ya mlipuko huo, amelaumu udhaifu katika idara ya ujasusi Kenya kwa kutoweza kutambua mipango ya mashambulio kama hayo kabla ya yafanyike, ili kuweza kuyatibua.

Akizungumza na BBC Abdulswamad amesema, 'Ni lazima tuweze kukubali kasoro iko wapi, ili tuweze kujua suluhisho litakuja vipi'.

Shabulio hilo limetokea wakati usalama umeimarishwa nchini Kenya kutokana na tisho la kutokea shambulio la kigaidi dhidi ya maeneo ya umma.

Katika siku za hivi karibuni Kenya imekuwa ikikabiliwa na mashambulio kadhaa katika maeneo mbali mbali nchini ukiwemo mji huo wa Mombasa na Nairobi, yaliosababisha vifo vya watu kadhaa na wengine wengi kujeruhiwa.

Ni hivi juzi tu watu 10 waliuawa huku zaidi ya hamsini walijeruhiwa katika milipuko miwili iliotokea katika Soko kubwa la nguo la Gikomba katika mji mkuu Nairobi.