WAWAKILISHI MARUFUKU KUJADILI KATIBA

SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho amepiga marufuku mijadala ya Bunge la Katiba, kuzungumzwa katika vikao vya Baraza la Wawakilishi.


Alisema hayo kutokana na kujitokeza kwa hoja mbali mbali zawajumbe, zinazozungumzia Bunge la Katiba, kiasi ya kuibua mijadala yenye muelekeo wa chuki na uhasama.

"Mimi ni mdau mkubwa wa umoja na mshikamano wa wananchi wa Zanzibar, sitaki kusikia lugha zenyekuashiria chuki na uhasama na kuwagawa wananchi wanaoishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," alisema.

Swali lililoibua hisia za Bunge la Katiba, liliulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Saleh Nassor Juma aliyesema kwamba hotuba ya Rais Jakaya Kikwete katika Bunge la Katiba, ndiyo chanzo cha kuvurugika kwa bunge hilo.


Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, alisema katika hotuba yake Rais Kikwete alitoa tahadhari kwa Watanzania kuhusu hatari ya kugawanyika kwa taifa hili, kama Muungano utavunjika.

Akifafanua, Aboud alisema kauli zawajumbe wa pande mbili, ndiyo zilizozusha mijadala, ambayo iliegemea matusi na baada kupelekea wajumbe wa vyama vya siasa vya upinzani kugomea vikao.


Mapema, Kificho alisema kuanzia sasa swali la mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, litakaloelekea masuala ya Bunge la Katiba, litazuiliwa na halitosomwa.

Aliwataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kuchangia na kutoa maoni ya Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maslahiya wananchi wa pande mbili huku wakiyapatia ufumbzi matatizo ya wananchi.