INTER MILAN KUKIPIGA DHIDI YA KENYA

Kwa mara ya kwanza klabu mashuhuri duniani Inter Milan ya Italia inazuru bara laAfrika.

Inter inatarajiwa kuwasili nchini Kenya kesho kwa mechi yao ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa Harambee Stars Jumapili, kama anavyotueleza mwaspoti wa BBC John Nene.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa shirikisho la kandanda nchini Kenya Sam Nyamweya klabu hiyo ya Italia Inter Milan inawasili Nairobi siku ya Ijumaa na kisha ipambanena Harambee Stars Jumapili kwenye mechi ya kimataifa ya kirafiki kuanzia saa kumi za afrika mashariki.

Ziara ya Inter inatokana na ushirikiano mpya kati ya shirikisho la kandanda nchini Kenya na lile la Italia.

Wengine ambao wamechangia kwa ziara hiyo ni wizara ya michezo, bodi ya utalii nchini Kenya na wasimamizi wakuu wa uwanja wa Kasarani.

Shirikisho la kandanda la Kenya hatahivyo halijataja kikosi cha Inter kwa ziara hii lakini wamesema mabingwa hao wa ligi ia Italia serie A mara 18 watakua na wachezaji wake wa kutegemewa.

Tayari mmoja wa nyota ya Inter MacDonald Mariga wa Kenya yuko Nairobi akijiandaa kwa mechi hiyo.

Mariga aliiwakilisha Harambee Stars wikendi iliyopita kwenye mechi yao yakufuzu kwa finali ya mechi za kombe la Afrika dhidi ya Comoros katika uwanja wa taifa wa Nyayo..

Inter ina mchezaji mmoja tu kwenye kikosi cha timu ya Italia cha kombe la dunia nchini Brazil, naye ni mlinzi Andrea Ranocchia aliye kwenye idadi ya wachezaji 30 ambao watapunguzwa hadi 24..


Haijulikani kama mshambuliaji matata wa Inter Diego Milito yuko kwenye ziara ya Kenya kwani tayari anaondoka Inter baadaya kukitumikia klabu hicho kwa miaka mitano.

Mashabiki wengi hawatamsahau Milito alipofunga mabao mawili yaliyoiwezesha Inter kuicharaza Bayern Munich mabao 2-0 katika mechi ya fainali ya kombe la mabingwa wa ligi ya ulaya mwaka 2010.

Msimu uliopita Milito, mwenye umri wa miaka 34, hakuonyesha mchezo mzuri kutokana na majeraha ambayo yamemsumbua kwa miaka ya hivi karibuni.

Miongoni mwa wachezaji wengine wanaoondoka ambao Milito alikua nao wakishinda Bayern ni Javier Zanetti, Esteban Cambiasso na Walter Samuel..

Inter pamoja na Manchester United ndizo timu mbili ambazo zimeshinda kombe la mabingwa wa ligi ya ulaya mara tatu.