ASHIKILIWA KWA KUNAJISI MTOTO MSIKITINI

Mkazi mmoja wa Mtaa wa Mungurumu, wilayani Liwale mkoani Lindi, anashikiliwa na polisikwa tuhuma ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka tisa anayesoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Kawawa.

Tukio hilo lilitokea jana baada ya mtuhumiwa kumchukua mtoto huyo na kumwingiza msikitini na kumfanyia kitendo hicho cha kinyama huku akimshikisha Kitabu Kitukufu cha Quran (Msahafu).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi, Renatha Mzingaalisema mtuhumiwa anashikiliwa na muda wowote atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Akizungumzia tukio hilo, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Wilaya Liwale, Hemedi Ndimbu alisema mtuhumiwa alimchukua mtoto huyo juzi saa nne asubuhi na kumpeleka msikitini ambako alimlazimisha kufanya kitendo hicho, huku akimshikisha Quran kwa kumlaghai kuwa kwa vile ameshika kitabu hicho kitukufu, akitoboa siri ya kitendo alichofanyiwa atakufa papohapo.

Ndimbu alisema baada ya mtoto huyo kufanyiwa kitendo hicho, alitoka huku akichuruzika damu sehemu za siri, hali iliyowafanya wanafunzi wenzake wamuulize lakini hakuweza kutoa jibu kutokana na kuhofia kufa.

Alisema baada ya muda mwalimu wa zamu ambaye alikataa kutaja jina lake alimwita na kumhoji, ndipo aliposema kuwa amefanyiwa kitendo hicho ndani ya msikiti, upande wa kinamama kwa kulazwa chini.

Katibu huyo amelaani kitendo hicho kufanywa msikitini na kutumia kitabu kitukufu kwenye tendo hilo la kinyama na kuiomba Serikali kumchukulia hatua kali mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.