Watu wengine 7 raia wa Kenya hawajulikani waliko. Shambulio hilo la Jumatatu limetokea siku moja baada yajeshi la anga la Kenya kuvamia kwa makombora maeneo yanayoshukiwa kuwa ngome za wapiganaji hao wa kiislamu, upande wa Somalia.
Bado Kundi hilo halijatoa taarifa yoyote kukana au kukiri kuhusika katika shambulio hilo.
*Washambuliaji
Akizungumza na BBC, Seneta wa kaunti ya Mandera iliyoko mpaka wa Kenya na Somalia Billow Kerrow, amethibitisha kuwa washambuliaji hao walitoka upande wa Somalia.
Amesema kuwa inashukiwa kuwa walikuja kuiba miraa kutoka kwa wafanyibiashara wa zao hilo upande wa Kenya, na walipofumaniwa na askari wa Kenya ndipo waliwafyatulia risasi.
Seneta Kerrow amekanusha madai kuwa huenda shambulio hilo linahusika na uhasama wa kikabila na kiukoo ulioko kati ya jamii zinazoishi katika mpaka huo.
Shabulio hilo limetokea wakati usalama umeimarishwa nchini Kenya kutokana na tisho la kutokea shambulio la kigaidi dhidi ya maeneo ya umma.
*Usalama
Ubalozi wa Marekani nchini Kenya umepunguza wafanyikazi wake na kuongeza ulinzi, huku Uingereza ikiimarisha usalama katika ubalozi wake na hata kuwaondoa baadhi ya raia wake waliokuwa nchini Kenya kwa usalama wao.
Wanamgambo wa Al shabaab wamezidisha mashambulio nchini Kenya tangu nchi hiyo iingize wanajeshi wake ndani ya Somalia kuwasaka wapiganaji hao haramu mwaka wa 2011