Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma jana, CAG Ludovick Utouh alivitaja vyama ambavyo havina akaunti benki kuwa ni UMD, NLD, NRA na ADC.
"Katika hesabu walizotuletea kulikuwa hakuna ushahidi kwamba wanaendesha akaunti benki," alisema huku akibainisha kuwa kitendo hicho ni kinyume na Kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Vyama vya Siasa.
Halikadhalika katika ukaguzi huo, vyama vya siasa 11 kati ya 21 vyenye usajili wa kudumu, havikuwasilisha taarifa za hesabu zamwaka kama Kifungu cha 14(1) cha sheria hiyo ya mwaka 1992 kinavyosema.
Alipoulizwa baadaye vyama hivyo, Utouh alivitaja CCK, UPDP, Tadea, Demokrasia Makini, Chausta, DP naAFP. Vyama vya Sauti ya Umma na Chauma viliwasilisha hesabu zao vikiwa vimechelewa.
Utouh alisema katika ukaguzi huo, taarifa za hesabu zilizowasilishwa na vyama 10 hazikufuata misingi yamfumo wa utoaji wa taarifa za fedha za kimataifa.
"Tulibaini kuwa hakuna chama cha siasa hadi sasa kilichowasilisha kwa msajili wa vyama vya siasa tamko lamali zote zinazomilikiwa na chama husika jambo ambalo ni kinyume cha sheria," alisema.
Utouh alitumia mkutano wake huo na wanahabari kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto kwa kusimama kidete kuhakikisha vyama vya siasa navyo vinakaguliwa na CAG kama sheria inavyoelekeza.
Kwa upande wake Zitto, naye alimpongeza CAG kwa kukagua vyama vya siasa akisema ni kati ya maeneo yaliyokuwa na matatizo.
"Kwa kitendo chako cha kuamua kukagua bila hata ya kupewa fedha ni kitendo ambacho kinaonyesha uzalendo wako wa hali ya juu," alisema Zitto na kuongeza:
"Kwa sababu tunachokitaka sisi ni kila senti ya mlipa kodi ikaguliwe na kama nilivyowahi kusema huko nyuma kwa miaka minne vilikuwa vimepewa ruzuku ya Sh69 bilioni."
Zitto alihoji kama CAG anakwenda kukagua bodi za mazao nchini ni kwa nini vyama vya siasa visikaguliwe wakati ndivyo vinavyozalisha Serikali pale vinaposhinda uchaguzi?