MBEYA CITY NDANI YA MASHINDANO YA NILE

Timu ya Mbeya City imeteuliwa kushiriki mashindano ya Shirikisho la Baraza la Vyama Vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) yajulikanayo kama Kombe la Mto Nile (Cecafa Nile Basin) yatakayofanyika nchini Sudan kuanzia Mei 22 hadi Juni 4 mwaka huu.


Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye alitangaza uteuzi huo kwa waandishi wa habari jijini Mbeya mara baada ya kufanya kazi ya kukagua Uwanja wa Sokoine kama unafaa kuchezewa mechi za kimataifa, akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi.


Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, mashindano hayo mapya hushirikisha timu zilizoshika nafasi ya pili katika ligi za nchi wanachama, ambapo kwa Tanzania, Yanga ndiyo ilitakiwa kushiriki michuano hiyo, lakini walisema hawapo tayari kushiriki.

Alisema kuwa hata walipoiteua timu ya Azam ambayo ndiyo mabingwa wa Ligi ya Tanzania Bara waligoma kushiriki wakidai kuwa wachezaji wao wapo likizo.


Alisema kuwa Cecafa kwa kushirikiana na TFF waliona ni vyema kuiteua Mbeya City ambayo imeshika nafasi ya tatu.