VIPIMO, MATIBABU YA DENGUE BURE

WANANCHI wa Mkoa wa Dar es Salaam wametakiwa kwenda katika hospitali za Serikali wanapohisi dalili za ugonjwa wa denge, kwa kuwa matibabu hutolewa bure wakati Serikali ikijiandaa kusambaza vifaa vya kupimia ugonjwa katika wilaya zote nchini.

Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal akifungua Kongamano la Pili la Kisayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), alisema Serikali haina mzaha katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa denge.

Alisema Serikali imeamua kusambaza vipimo hivyo, baada ya kuonekana kuwa ni tishio kwa maisha ya binadamu hivyo serikali imejipanga kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa.

"Kutokana na ukubwa wa tatizo hili, tayari Serikali imejipanga kipambana na ugonjwa huu, ndio maana sasa tumeandaa mkakati wakusambaza vifaa vya vipimo vya ugonjwa huu kwa kupitia wilaya zote nchini," alisema Dk Bilal.

Akizungumzia masuala ya utafiti nchini, Bilal alisema wanaweka mikakati kuongeza rasilimali watu hasa vijana katika masuala ya utafiti ikiwemo katika masuala ya afya, ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi tafiti hizo.

*Muhas

Awali Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Ephata Kaaya, alisema chuo hicho kimeandaa kikosi kazi maalumu kwa ajili ya kufanya utafiti kuhusu ugonjwa huo, ambacho kitashirikiana na watafiti wengine.

Profesa Kaaya alisema lengo la kongamano hilo ni kutafakari na kuangalia malengo waliyojiweka chuoni hapo hasa katika masuala ya utafiti kama yamefanikiwa katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu na nini kifanyike katika kukamilisha yale yalisalia.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Profesa John Mkoma, alisema kwa sasa Mamlaka yake kupitia Muhas na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wameanza kutumia simu za mkononi kwa ajili ya kufikisha taarifa mbalimbali kwa wananchi kwa njia ya ujumbe mfupi.

Alisema lengo la kutumia simu za mkononi, ni kutoa taarifa kwa haraka kwa wananchi juu ya masuala mbalimbali ya afya yanayotokea, ikiwemo magonjwa ya milipuko kwa nia ya kupunguza maambukizi kwa haraka.

Dar es Salaam

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alisema matibabu ya denge yanatolewa bure na kuwataka wananchi wakijisikia dalili, kwenda katika hospitali za Serikali.

"Tunaomba wananchi wanapohisi dalili za ugonjwa huo kwenda katika hospitali za Serikali, ambazoni Amana, Mwananyamala na Temeke kwa kuwa matibabu yanatolewa bila malipo," alisema Sadiki alipokuwa akizungumzia gharama za matibabu ya homa hiyo.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kwa sasa wanajenga uwezo ili kila wilaya iwe na vituo vitano kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa huo.

*Dawa

Sadick aliongeza kuwa Serikali itanyunyuzia dawa ya (Lavacide) sehemu za mikusanyiko kama vile mashuleni na kwenye madimbwi, lakini maeneo ya hotelini na mabaa watapaswa kunyunyuzia dawa kwa gharama zao.

"Kwa upande wa wizara, idara na taasisi za Serikali wanapaswa kunyunyuzia dawa kwa gharama zao, (yaani matumizi mengineyo)," alisisitiza huku akisema hata kwenye ofisi yake wamefanya hivyo kwa gharama zao.

Sadiki aliwataka viongozi wa mitaa na watendaji wengine kuwahimiza wananchi kuhusu usafi wa mazingira ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.

Alisema wananchi wanapaswa kuhakikisha vifuu vya nazi na visoda kwani maji kidogo yanayokaa katika vitu husababisha mbu wanaosababisha ugonjwa huo kuzaliana. Alisisitiza hatua ya kwanza kuzuia ugonjwa huo ni usafiwa mazingira na dawa ni hatua ya mwisho.

*Ushauri

Katika hatua nyingine, Serikali imeshauriwa kuwapa semina waganga wa tiba mbadala kuhusu hali halisi ya ugonjwa huo, ili kuepuka kuibuka kwa wataalamu watakaodai wanatibu na kuwafanyia majaribio wagonjwa.

Ushauri huo ulitolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mandai Herbal Clinic, Dk Abdallah Mandai, wakati akizungumzia ugonjwa wa denge na kuongeza kuwa umekuwa ni tatizo la kitaifa linalohitaji hatua stahiki za kukabiliana nalo.

*Dalili

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo, alisema dalili zaugonjwa huo ni kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu na dalili hizo huanza kujitokeza kuanzia siku 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya denge.

"Kwa wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana na dalili za malaria, hivyo basi tunawaomba wananchi wakipata homa kuhakikisha wanapima kama wana malaria au la, ili hatua stahiki zichukuliwe," alisema Pallangyo.

Aidha aliongeza kuwa kuna aina tatu tofauti za ugonjwa huo katika namna unavyojitokeza, iwapo mtu aking'atwa na mbu mwenye virusi hivyo.

Aina ya kwanza ndio homa ya denge yenyewe, ambayo huambatana na dalili kuu tatu za homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo au uchovu. Kwa Tanzania mpaka sasa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wamejitokeza wakiwa na dalili hizo.

Aina ya pili ni denge ya damu, ambayo huambatana na dalili za magonjwa kutokwa na damu kwenye fizi au puani na kutokwa nadamu chini ya ngozi. Iwapo mgonjwa huyo ataumia sehemu yoyote, ni rahisi kupoteza damu nyingi kupitia kwenye michubuko.

Aina ya tatu ni denge ya kupoteza fahamu, ambayo huambatana na mgonjwa kupoteza damu nyingi ambayo husababisha mgonjwa kupoteza fahamu.

Mpaka sasa dalili hizo zimeonekana kwa mgonjwa mmojakati ya wagonjwa 400 waliokwishwa thibitika kuwa na ugonjwa hapa nchini.