ABDEL-FATTAH AL-SISI RAIS MPYA MISRI

Rais mpya wa Misri Al Sisi
Aliyekuwa mkuu wa jeshi nchini Misri , Abdel-Fattah al-Sisi, ndiye Rais mpya wa Misri baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika wiki hii.
Vyombo vya habari vya kitaifa nchini Misri vinasema matokeo ya mapema yanaonyesha kwamba amejinyakulia zaidi ya asilimia 96 ya kura hizo.
Muslim Brotherhood na makundi mengine yaliususia uchaguzi huo na idadi ya waliojitokeza kupiga kura inakadiriwa kuwa chini ya asilimia 45.
Hii ni licha ya kuongezwa siku ya kupiga kura, kutangazwa siku ya kitaifa ya mapumziko na hata pia kutolewa usafiri wa bure kuwapeleka wananchi kupiga kura.
Sisi alimng'oa mamlakani aliyekuwa Rais Mohammed Morsi ambaye alikuwa Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri.
Sherehe za baada ya kutangzwa ushindi wa Al Sisi

'Vita dhidi ya Brotherhood'
Aliongoza vita dhidi ya vuguvugu la Muslim Brotherhood, lake Mohammed Morsi ambapo wanachama zaidi ya 1,400 waliuawa na wengine 16,000 kuzuiliwa.
Vuguvugu la Brotherhood lilisusia uchaguzi huo,kama walivyofanya wanaharakati wa makundi mengine ya kisiasa.
Hamdeen Sabahi, mgombea mwengine wa pekee katika uchaguzi huo,alisema hapo awali kuwa chama chake kilishuhudia ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi.
Hata hivyo alikatalia mbali wito kutoka kwa wafuasi wake kujiondoa katika uchaguzi akisema kuwa jambao kama hilo lingekiuka matakwa ya wamisri.
Sabahi alipata kura 760,000 kati ya kura milioni 24.7 zilizohesabiwa , na kushindwa katika maeneo mengi ya nchi ambako kura nyingi zilizopigwa zilikuwa na makosa.
Shughuli ya kuhesabu kura ikiendelea

Mamia ya wafuasi wa Sisi walisherehekea ushindi wake mjini Cairo nyakati za asubuhi na mapema, wakipeperusha bendera za Misri huku wakipiga honi kwa fujo.
Maafisa wa uchaguzi waliongeza muda wa kupiga kura kwa siku nyingine moja na ya tatu kwa matumaini kuwa wangepata idadi kubwa ya wapiga kura.
Licha ya hilo vituo vingi vya kupigia kura viliripotiwa kutokuwa na watu Jumatano.