Akizungumza kabla ya kutia saini makubaliano ya msaada huo jijini Arusha jana, Balozi wa EU nchini, ambaye pia ni Balozi wa Jumuiya hiyo kwenye Sekretarieti ya EAC, Filberto Sebregondi alisema wametoa fedha hizo kuimarisha usalama Ukanda wa Pwani wa EAC kutokana na umuhimu wake kibiashara.
"Licha ya kuhatarisha usalama, vitendo vya uharamia ni kikwazo cha maendeleo ya kibiashara kati ya Afrika na Ulaya, hatuna budi kuyakabili kwa pamoja," alisema Balozi Sebregondi
Msaada huo ni sehemu ya Euro 37.5 milioni kusaidia vita dhidi ya maharamia na uhalifu wa majini katika nchi za Ukanda wa EAC, COMESA, IGAD na IOC. Pamoja na kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama, fedha hizo pia zitatumika kuimarisha vyombo vya uamuzi.