YINGLUCK SHINAWATRA ATIMULIWA UWAZIRI MKUU

Mahakama ya kikatiba Nchini Thailand imeamuru Waziri mku wa Nchi hiyo Yingluck Shinawatra kuondoka madarakani baada ya kumkuta na hatia ya kutumia vibaya mamlaka yake.


Alifikishwa mahakamani hapo jana Jumanne na akakanusha madai kwamba alimfuta kazi mkuu wa usalama wa taifa na mahala pake akamweka mwandani wa chama chake Thawil Pliensri mnamo mwaka wa 2011.

Mapema leo alirejeshwa tena mahakamani na ndipo uamuzi huo ukatolewa.


Katika uamuzi wake, mahakama imesema kuwa Bi Yingluck alikiuka katiba alipomhamisha afisa huyo mkuu wa serikali mwaka 2011.

Aidha mahakama pia imewaamuru baadhi ya mawaziri waliohusika katika uhamisho huo kujiuzulu nyadhifa zao.


Thailand imekuwa katika mikwaruzano ya kisiasa katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Waandishi Habari wanasema kuwa hatua hiyo ya mahakama huenda ikafanya mambo kuwa mbaya zaidi.