Aidha, Muswada wa Haki ya Kupata Habari, utafiti wake umekamilika na unaandaliwa na wizara ya katibana sheria na baada ya maamuzi utafikishwa bungeni kujadiliwa na kuwa sheria.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia aliliambia bunge jana wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya (CCM) aliyetaka kujua ni lini serikali itapeleka miswada hiyo miwili na kujadiliwa kisha kuwa sheria.
Alisema ni kweli mwaka 2007, serikali iliitikia mwito wa wadau mbalimbali wa habari, waliotaka kuwepo na tofauti za sheria ya huduma ya vyombo vya habari na uhuru wa kupata habari.
"Serikali imepokea mapendekezo kutoka kwa wadau, nafurahi kulijulisha bunge lako tukufu kuwa muswada wa sheria ya kusimamia vyombo vya habari, umekamilika baada ya kupitia hatua zote muhimu za kuandaa muswada na taratibu za kuletwa bungeni zinaandaliwa," alisema.
Katika swali la nyongeza, mbunge wa Nchinga, Saidi Mtanda(CCM) alitaka kujua ni lini muswada utaletwa bungeni baada ya kuombwa kwa miaka 17 na kusababisha mazingira ya uhuru wakupata habari kuwa na changamoto.
Akimjibu, Nkamia alisema muswada huo utapelekwa wakati wowote kuanzia sasa, kwa kuzingatia kalenda za bunge la bajeti na wakati wa muswada.
Mtanda aliungwa mkono na mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR -Mageuzi) na Mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu Vullu (CCM) waliotaka kujua muda maalumu wa muswada huo kufikishwa bungeni na kuhoji vyombo vya habari vinapokosea wanashtakiwa kwa sheria gani na hakuna sheria.
Nkamia alisema akiwa mdau wa habari, atahakikisha kuona waandishi wa habari wanapata haki zao hivyo utapelekwa bungeni lakini kila jambo lina utaratibu wake.