Akizungumza jana na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule, alisema misaya kumuaga Balozi Flossie itafanyikaleo katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Balozi Flossie alifariki Ijumaa iliyopita akiwa njiani wakati akipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu, baada ya kuugua akiwa nyumbani kwake.
Kwa mujibu wa Haule, Jumatatu iliyopita usiku, Balozi Flossie alijisikia vibaya na kupelekwa Aga Khan ambako alipatiwa matibabu nakuwekwa mapumziko kati ya saa sita usiku saa 12 asubuhi, ambapo alipatiwa dawa za kutumia nyumbani na kuruhusiwa.
Hata hivyo, Haule alisema Ijumaa iliyopita, hali ilibadilika mchana na kurejeshwa hospitalini, lakini alipofikishwa Aga Khan, madaktari walimfanyia vipimo na kubaini ameshafariki.
Sababu ya kifo Haule alisema mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi jana, ambapo madaktari walibaini kuwa chanzo cha kifo chake ni kuvimba na kupasuka kwa mshipa mkubwa wa moyo, uliosababisha damu kujaa na kwenye mfuko wa moyo na kushindwa kufanya kazi.
Haule alisema wakati wa uhai wake,Balozi Flossie alifanya kazi zake kwa kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi na kushirikiana vizuri na mabalozi wenzake wanaowakilisha nchi zao Tanzania.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Leo utapelekwa ukumbi wa Mwalimu Nyerere kwa misa na kuaga kabla ya kusafirishwa kesho kwenda nyumbani kwao, Blantyre, Malawi kwa ajili ya maziko, yatakayofanyika Jumatano wiki hii.