STARS KUMENYANA NA MALAWI TENA

TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars inatarajiwa kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki na Malawi (Flames) keshokutwa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwenye vyombo vya habari jana, mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni.

Stars ilishacheza mechi ya kirafiki na Malawi kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya mwezi uliopita na kutoka suluhu.

Mechi hiyo itakuwa ya mwisho kwa Stars kujipima kabla ya kucheza mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika dhidi ya Zimbawe mjini Harare Juni mosi mwaka huu.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Stars ilishinda bao 1-0, matokeo ambayo yana ilazimisha kufanya jitihada ama kulinda bao hilo ama kuongeza ili kusonga mbele.

Mshindi wa mechi hiyo atacheza na mshindi wa mechi kati ya Msumbiji na Sudan Kusini ambapo katika mechi ya kwanza Msumbiji ilishinda mabao 5-0.

Stars ipo kambini Tukuyu mkoani Mbeya chini ya Kocha wake Mart Nooij kujiandaa kwa mechi hizo.

Malawi iliwasili jana mchana na msafara wa watu 27 Flames inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Malawi, Young Chidmozi inatarajia kufanya mazoezi leo jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Baada ya mechi hiyo, Malawi itakwenda moja kwa moja nchini Chad kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika itakayochezwa Mei 30 mwaka huu jijini Ndjamena.