Katika vurugu hizo, ambazo zililazimisha polisi kurusha mabomu ya machozi ili kuwatawanya waandamanaji, pia mali mbalimbali ziliharibiwa, likiwemo gari la Mbunge wa Tanga Mjini, Omary Nundu.
Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, David Misime alisema vurugu hizo zilitokea juzi saa 7.30 mchana katika Mji mdogo wa Kibaigwa. Alisema jumla ya watu 34 wanashikiliwa wakihusishwa na vurugu hizo.
Misime alisema vijana wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 300, wakishirikiana na wabeba mizigo wa Soko Kuu la Mazao la Kibaigwa walifanya maandamano bila kibali na kung'oa bango la Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Alisema bango lililong'olewa ni la tangazo la kuzuia wafanyabiashara kuingiza mazao sokoni bila kulipa ushuru uliowekwa kwa mujibu wa sheria.
Kamanda huyo alisema viwango vyaushuru vinavyotozwa vilipanda tangu Julai Mosi mwaka jana. Kwa mujibu wa viwango vipya, ushuru wa gunia la kilo 100 za karanga ulipanda kutoka Sh1,000 hadi Sh3,000, gunia la mahindi kutoka Sh500 hadi Sh1,000, dumu la mafuta ya alizeti lilianza kutozwa Sh500, gunia la mashudu Sh1,000 na gunia la alizeti Sh1,000. Viwangohivyo vinapingwa na wabeba mizigo.
"Vijana hao wabeba mizigo walifanya fujo kwa kufunga Barabara kuu ya Dodoma – Morogoro kwa mawe na kuchoma matairi, pia walivamia maduka na baa za jirani na kupora vinywaji na kuvunja majokofu na kusababisha uharibifu mkubwa," alisema Misime.