TABORA WAMGOMEA SHEIKH MKUU

Kutokana na kuondolewa kwa Sheikh wa Mkoa wa Tabora, Shaaban Salum na Mufti wa Tanzania, Sheikh Shaaban Issa bin Simba, baadhi ya Waislamu wamedai kitendo hicho hakivumiliki.

Sheikh Salum alivuliwa uongozi na kupewa barua iliyosainiwa na Sheikh Simba inayoeleza kuwa ameshindwa kutekeleza matakwa ya kufuta usajili wa Msikiti wa Ijumaa kutoka kwa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) baada ya kupewa miezi mitatu kufanya hivyo.

Akizungumza kwenye Msikiti wa Ijumaa baada ya Swala ya Alasiri, Sheikh Salum aliwaeleza waumini kuwa amevuliwa uongozi kutokana na mkakati wake wa kuwaendeleza Waislamu.

"Nimesimama kuwaeleza kuwa nimekumbwa na kadhia leo (jana), pengine nitabaki kuwa imamu kwani nimevuliwa uongozi siyo tena Sheikh wa Mkoa kutokana na mkakati na mpangokazi wangu wa maendeleo ambao umesababisha kuvuliwa madaraka," alisema Sheikh Salum.

Alisema alikuwa na mipango ya kujenga maduka kuzunguka msikiti na kwamba ana uhakika wameweza kupata Sh10 milioni ambazo zitatumika kwa manufaa ya Waislamu.


Sheikh Salum aliwalaumu watu wasiowatakia mema ambao alidai wamejaa husuda, huku akiwaita waongo na wanafiki duniani na ahera.

Akitoa msimamo wa Waislamu wanaoswali msikiti hapo, msemaji wa msikiti huo, Abuu Bakari alisema hawatambui kuvuliwa uongozi kwa Sheikh Salum na kwamba wanaendela kumtambua.


"Tunatoa taarifa kwa Mufti, Waislamu hususani wa Msikiti wa Ijumaa kuwa tunamtambua Sheikh Shaaban Salum kama Sheikh wa Mkoa. Tunamtambua hivyo na tunamwagiza mufti alete mtu atueleze sababu za kumtoa kwenyewadhifa wake," alisema.


Bakari aliitaka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Seleiman Kumchaya kutoa taarifa za kuvurugwa kwa waumini wa Kiislamu, vinginevyo yatakayotokea asije akalaumu watu wa Tabora.


Baadhi ya waumini waliunga mkono tamko hilo na kudai wataendelea kumtambua kama kiongozi wao na kwamba Simba amevunja Katiba ya Bakwata na kutaka aondolewe kwenye wadhifa wake huku wakisisitiza Sheikh Salum alichaguliwa na Waislamu ambao ndiyo wanaopaswa kuelezwa makosa aliyotenda ili wamhukumu siyo kuondolewa kinyemela.


"Kama mufti ameona Sheikh Salum amefanya makosa kwa nini hakuchagua mtu miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Ulamaa, badala yake amechagua mtu kutokanje ya baraza hilo?" alihoji Kansa Mbarouk.