PUTIN HATAKI KURA YA MAONI

Katika hatua ambayo haikutarajiwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ametoa wito kwa makundi yanayotaka kujitenga wanaounga mkono Urusi Kusini Mashariki mwa Ukraine waahirishe kura ya maoni ya Jumapili juu ya kutaka kujitenga kama hatua muhimu kuimarisha mashauriano ya amani kati ya makundi yanayozozana nchini humo.

Rais Putin alisema kuwa hatua hiyo itaimarisha mazingira ya kufanya mashauriano kati ya Serikali ya Ukraine na wale nchini wanaopendelea Urusi wanaotaka maeneo yao kujitenga na kuungana na Urusi.

Amesema kuwa uchaguzi wa Urais uliopangwa kufanywa Mei 25, ni hatua inayofaa.

Siku chache zilizopita Bwana Putin alitaja uwezekano wa kuwa na uchaguzi huo wa Urais kama upuzi mtupu.

Lakini katika taarifa ya hivi sasa Bwana Putin amesema uchaguzi huo hautakuwa na maana iwapo raia wote wa Ukraine hawatahusishwa na kuwahakikishia jinsi haki zao zitakavyolindwa baada ya uchaguzi.


Vladmir Putin pia alidai kuwa Urusi imewaondoa wanajeshi wake kwenye mpaka wake na Ukraine.

Hata hivyo mataifa ya Magharibi yanatarajiwa kutoamini hakikisho hili hadi watakapo shuhudia kinachoendelea mpakani.


Mataifa hayo pia yanasubiri kuona iwapo taarifa ya Putin itapunguza uhasama miongoni mwa wananchi wa Ukraine.