DEREVA AFARIKI AKIWA KATIKA FOLENI

Dereva wa malori ya safari za masafa marefu Charles Mbungu (46), amefariki dunia akiwa ndani ya lori alipokuwa katika foleni ya ukaguzi wa magari kwenye Kituo cha Misugusugu, Kibaha, Pwani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema dereva huyo aliyekuwa alikitoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), alikutwa na mauti hayo akiwa ndaniya gari aina ya Leyland Daf alilokuwa akiendesha kuelekea Dar es Salaam.

Kamanda Matei alisema kabla ya dereva huyo mwenyeji wa Mkoa waIringa kabla ya kufikwa na mauti, alikuwa akilalamika kuwa anajisikia vibaya walipokuwa njiani.


Akizungumzia tukio hilo utingo wa lori hilo, Said Hemed (22) alisema:

"Tulianza safari vyema, lakini tulipokaribia Chalinze, akaanza kulalamika kuwa hajisikii vizuri. Tuliendelea na safari, huku nampa moyo lakini alirudia maneno hayo tulipofika Mlandizi, lakini alikuwa akinieleza itambidi kwenda kupimapindi akifika tu Dar es Salaam."

Tukaendelea na safari na jamaa alikua safi tu akiendesha, lakini tulipokuwa kati ya Mlandizi na Kibaha alirudia kusema mwili wake kama haupo vizuri vile na tulipokuwa katikati ya safari kabla ya kufika Misugusugu aliniambia... 'Dogo hali siyo nzuri ninaumwa aisee'.


"Nikamuuliza sasa kuendesha utaweza kweli? Akaniambia Mungu ni mwema, nitajitahidi tufike Dar es Salaam ili nikafanye vipimo kabisa maana hali siyo nzuri. Tukajahadi hapa check point (kituo cha ukaguzi) sasa akawa ananieleza huku kalalia usukani. Mimi nikateremka kuangalia kinachoendelea, kwani ilikuwa foleni ndefu kiasi. Muda mfupi nikarudi kwenye gari, kufika nikamkuta 'bro' amefariki, yaani ni kama kaniambia hebu nipishe naondoka. Sikuamini lakini ndivyo ilivyotokea."

Kamanda Matei alisema kuwa mwiliwa marehemu ulichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Tumbi kwa ajili ya kuhifadhiwa pamoja na kufanyiwa uchunguzi.


Ofisa Habari wa Hospitali ya Tumbi, Gerald Chami alisema vipimo vilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi.

Hemed alisema baadaye kuwa baada ya tukio hilo alifanya utaratibu wa kuliingiza lori hilo katika yadi ya magari iliyopo eneo hilo na baadaye kufanya mawasiliano na tajiri yake kwa ajili ya utaratibu wa kuuhifadhi mwili pamoja na gari.