ASILIMIA 48 YA WAKAZI WA MPANDA HUPATA MAJI SAFI

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Agrey Mwanri, amesema ni asilimia 48 tu ya wakazi wa Wilaya ya Mpanda, ndio wanapata maji safi na salama.


Alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa MpandaVijijini, Moshi Kakoso (CCM) bungeni jana, aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kumaliza tatizo la maji katika vijiji vya Kamsanga, Bugwe, Sibwesa, Mpemba, Kabage, Mwese na Bujombe.


Kutokana na hali hiyo, alisema bado ipo changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo ya maji kwa wakazi wa wilaya hiyo na ili kutatua tatizo la maji katika vijijihivyo, Serikali itatekeleza mradi wa maji wa kisima kifupi katika Kijiji cha Kamsanga na tayari upimaji wa eneo la kuchimba kisima kirefu umefanyika na kitachimbwa Juni mwaka huu.

Alisema Kijiji cha Bujombe katika mwaka 2013/14 kimetengewa Sh milioni 8 kwa ajili kuchimba kisimakifupi kimoja."


Katika Kijiji cha Mwese, Serikali kwa kushirikiana na Kanisa Katoliki katika mwaka 2013/14, imepanga kutumia Sh milioni 65 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji mserereko utakaowahudumia wananchi wengi zaidi ukiwa na vituo vitano.

"Aidha, kijiji hiki pamoja na kijiji ya Mpemba vimeingizwa katika mpango wa kuleta Matokeo Makubwa Sasa (BRN), ambapo miradi yenye thamani ya Sh bilioni 1.4 inatarajiwa kujengwa ifikapo 2015/16,"alisema Mwanri.

Alisema hadi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda imepokea Sh milioni 742 kwa mwaka wa fedha 2013/14, fedha ambazo zitatekeleza miradi yote ya maji.


Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kufuatilia kwa karibu kiasi chote cha fedha kilichobaki, ilikipatikane kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2013/14.