VIONGOZI wa kitaifa wameonya kuhusu muelekeo wa mchakato wakupata Katiba mpya, kwamba usiachiwe kuvuruga amani, upendona mshikamano wa kitaifa, huku Rais Jakaya Kikwete akihadharisha kuwa isipopatikana, Katiba hiyo, itatafutwa tena miaka ijayo.
Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, akikabidhi nyumba 30 za watumishi wa afya wa Mkoa wa Singida, zilizojengwa kwa ufadhili wa Global Fund Round9 na kusimamiwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa juzi, aliwataka Watanzania kuhakikisha mchakato wa Katiba mpya unaoendelea hivi sasa, hauvurugi amani, upendo na utulivu uliopo nchini.
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, akihutubia katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi janaBwawani Zanzibar, alisema zipo dalili kuwa baadhi ya wanasiasa wameanza kuutumia mchakato wa Katiba mpya vibaya, kwa kuanza kujenga uhasama wa kisiasa ambaohatma yake ni nchi kuingia katika machafuko.
Mkapa alisema amani na utulivu uliopo nchini kwa miaka mingi havina budi kudumishwa na kukuzwa, ili kuenzi waasisi wa Taifaletu.“
Vyovyote utakapoishia mchakato huu wa Katiba…amani, upendo na utulivu lazima vihimili maisha yetu,” alisema Mkapa na kuongeza:
“Tuhitilafianeni lakini bila kupigana.”
Tahadhari Zanzibar
Dk Shein kwa upande wake kutokana na dalili alizozibaini, amewatahadharisha wananchi na wanasiasa, kwamba mchakato wa kupata Katiba mpya usiwe chanzo cha kuvuruga amani na utulivu uliopo na kujenga uhasama.
Alisema kwa muda mrefu sasa Zanzibar imekuwa ikipata mafanikio makubwa, ikiwemo kuimarika kwa amani na utulivu ambao umewafanya wananchi kuishi vizuri kwa maelewano na kuzika tofauti za itikadi za kisiasa.
“Wananchi wa Zanzibar nawaasa kwamba Bunge Maalumu la Katiba lipo kwa mujibu wa Sheria na wananchi kamwe wasijenge chuki na uhasama utakao sababisha nchi yetu kurudi katika siasa za chuki nauhasama,” alisema.
Miaka ijayo Rais Kikwete akizungumza katika Sikukuu ya Wafanyakazi Dar es Salaam jana, aliwataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kutumia ipasavyo nyongeza ya siku 60 watakayopatiwa kwa kuja na uamuzi wenye manufaa kwa Watanzania, vinginevyo ikishindikana, Katiba hiyo, itatafutwa tena miaka ijayo.
“Mimi Rais kazi yangu nimemaliza ya kuteua wajumbe, sasa yanayoendelea mle ndani ni ya kwao…kwa kweli nasikitishwa na kilichokuwa kikijiri ndani ya Bunge lile na kuniacha na maswali kuwa hivi tusi ni hoja?” alihoji Kikwete.
Alisema kuteuliwa kwa wajumbe hao kutoka taasisi, itikadi na maeneo tofauti, ilikuwa ni moja yambinu ya kuibua mijadala mbalimbali ambayo ingewezesha kupatikana kwa Katiba nzuri yenye manufaa kwa Watanzania.
“Hata wazungu wanasema acha mawazo 100 yagongane ili kupatikane wazo moja la msingi, lakini naamini kuwa wajumbe hawa hawataishia pale, watakaa na kutumia likizo waliyonayo na kuja na mawazo mazuri na kutuletea Katiba mpya,” alisisitiza.
Aliwataka Watanzania kuwatumia wajumbe wanaowawakilisha katika Bunge hilo, kuwasilisha mawazo yao badala ya kuwaachia watoe mawazo yao jambo ambalo ni rahisi kwao kutekwa na mawazo ya wengine.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Nicholaus Mgaya, alisema shirikisho hilo, limesikitishwa na mwenendo wa Bunge hilo la Katiba, ambao umesababisha wananchi kupoteza imani nalo na kushauri wajumbe wote waliohusika na makosa yaliyojitokeza kujirekebisha katika Bunge lijalo.