WATU WAWILI WAFARIKI BAADA YA KIFARU KUGONGA NYUMBA

WATU wawili wamekufa baada ya gari la Kijeshi (Kifaru cha Jeshi la Wananchi Tanzania JWTZ) kupoteza mwelekeo na kuparamia makazi ya watu mkoani Lindi na kupelekea watu wengine saba kujeruhiwa vibaya.

Taarifa zilizoifikia FikraPevu leo na kuthibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani humo zinaeleza kuwa ajali hiyo imetokea saa 05:30 asubuhi katika eneo la Mnonela barabara ya Mingoyo-Mtwara na kuwa ajali hiyo ilihusisha gari namba 018 APC mali ya JWTZ kikosi namba 83 Reget.

Gari hilo lilikuwa likitokea mkoani Mtwara kuelekea katika wilaya ya Nachingwe mkoani Lindi kikazi ambapo lilikuwa likiendeshwa na Askari mwenye namba MT 99241 Priv. Shadhil Nandonde pia haijawekwa wazi kuwa ni kazi gani lilikuwa linaenda kufanya shughuli gani.

Imeelezwa kuwa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Askari mwenye namba MT 10728 Pr Pascal Komba na mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Somoe Kamtaule (75), mkulima wa eneo hilo aliyekuwa ndani ya nyumba.

"Lilipoteza mwelekeo na kuingia kwenye nyumba mbili na katika nyumba moja ilisababisha kifo cha mtu mmoja (mwanamke) na kwenye gari hilo Mwanajeshi mmoja alikufa pamoja na majeruhi saba kujeruhiwa vibaya".

Aidha, majeruhi katika ajali hiyo ni Askari mwenye namba MT 10744 Pr. Simon Edward, Askari namba MT 106842 Pr.Feruz Haji, Askari mwenye namba MT 1077263 Pr.Omary Makao pamoja na Askari mwenye namba MT 99018 Pr.Mbaruk Duchi.

Wengine ni Askari mwenye namba MT 107442 Pr. Simon Masele, Askari mwenye namba MT 107218 Pr.Ndekenya R na Askari mwenye namba MT 99241 Pr.Shadhil Nandonde ambaye alikuwa dereva.

Kwa mujibu wa Polisi mkoani humo, chanzo cha ajali hiyo kinachunguzwa na majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mtwara ya Ligula kwa ajili ya matibabu.

Wakati huo huo, watu 2 wameripotiwa kufa na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa, baada ya basi la Kampuni ya Super Feo kupinduka katika eneo la Sanangula nje kidogo ya mji wa Songea likitokea mkoani Ruvuma kwelekea mkoani Mbeya.

Majeruhi wa ajali hiyo wanatibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma, huku chanzo cha ajali hiyo kikiwa bado hakijafahamika.

Chanzo: Fikra Pevu