PIKIPIKI ZOTE KUSAJILIWA UPYA

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuanza kwa mfumo mpya wa usajili wa pikipiki zote nchini.

Usajili huo utakwenda sambamba na kubadilishwa kwa namba za pikipiki unaoanza na namba MC 101 AAA badala ya namba zinazotumika sasa.

Kwa mujibu wa taarifa ya TRA kwa umma, usajili wa mfumo mpya ambao uko kwa mujibu wa sheria, unatarajiwa kuanza Oktoba mosi, mwaka huu.

"Kwa mantiki hiyo, wamiliki wote wa pikipiki za magurudumu mawilina matatu wanajulishwa kuwa namba zote zitabadilishwa kuanzia Oktoba mosi mwaka huu, hivyo wamiliki wa vyombo hivyo wanatakiwa kufika katika ofisi za TRA kwa ajili ya utaratibu huo ," inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo, wamiliki wa pikipiki wametakiwa kulipia Sh 10,000 kama gharama za kubadilisha namba na kupewa kadi mpya ya umiliki wa chombo. Imeelezwa kazi ya kubadilisha namba kwa pikipiki zilizokwisha andikiwa itafanywa kwa miezi sita kuanzia Oktoba mosi na kwamba baada ya muda huo, ubadilishwaji utakwenda sambamba na adhabu.