KATIBA YA SASA KUREKEBISHWA, MGOMBEA BINAFSI RUKSA UCHAGUZI UJAO

MCHAKATO wa kuandika Katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu ujaoumekwama, baada ya viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge na Rais Jakaya Kikwete, kukubaliana kusitisha mchakato huo. Badala yake viongozi hao wa vyama vya siasa wamekubaliana kwamba Katiba ya sasa ya mwaka 1977, ipelekwe bungeni kufanyiwa marekebisho, ili kutoa fursa Uchaguzi Mkuu ujao ufanyike mwakani kisha mchakato wa Katiba mpya, uendelee baada ya uchaguzi huo.

Mambo ambayo vyama vya siasa wamekubaliana, ni kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi itakayosimamia uchaguzi wa mwaka 2015; mshindi wa uchaguzi wa Rais apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote, matokeo ya uchaguzi wa rais yaruhusiwe kupingwa mahakamani na kuruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi.

Pia vyama vingine vya siasa ambavyo vinataka kupendekeza mambo mengine ya kurekebisha katika Katiba ya mwaka 1977, vimeombwa kufanya hivyo mapema kwa kuwa muda uliopo wa kufanya mabadiliko ni mdogo.

Kutokana na mabadiliko hayo, TCD kupitia vikao vyake, itaratibu na kujadili mapendekezo hayo na kupeleka serikalini kwa hatua zingine za kuingiza mapendekezo hayo kwenye marekebisho ya Katiba.

"Muda tulio nao ni kwa mabadiliko yanayopendekezwa kujadiliwa katika Bunge la Novemba na wakichelewa Bunge la Februari 2015," alisema John Cheyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.

Kwa makubaliano hayo, kazi inayofanywa na Bunge Maalumu la Katiba (BMK) ya kuandika Katiba mpya itakoma Oktoba 4 mwaka huu, siku ambayo Bunge hilo litakuwa halijakamilisha uandikaji wa Katiba, ambao unafanywa na kamati ya uandishi iliyo chini ya Andrew Chenge.

Alipoulizwa kama Rais atakayekuja asipoona Katiba kama kipaumbele itakuwaje, Cheyo alisema yeye na viongozi wenzake wanaamini kuwa kiongozi huyo atashauriana na wenzake ili kukamilisha mchakato huo.

"Rais ana uhuru wake, tusimwekee masharti Rais ajaye," alisema Cheyo.

Hata hivyo hakuweka bayana kama mchato huo utaanzia pale ulipomalizikia au utaanza upya.

Uamuzi huo unakidhi baadhi ya madai ya kundi la Umoja wa Katibaya Wananchi (Ukawa) ambao ni wajumbe waliokuwa ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, lakini walijiondoa kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge hilo.

Kutokana na msimamo wao wa kutorejea bungeni hata baada ya kuombwa kufanya hivyo na viongozi mbalimbali, kundi hilo lilitia ngumu badala yake wakataka kukutana na Rais Kikwete.

Miongoni mwa madai yao waliyokuwa wanayataka ya kusitisha Bunge hilo hayakufanikiwa kwani litaenda hadi mwisho kwa kuwa lipo kisheria.

Ratiba ya Bunge inaonesha kuwa majadiliano ya wabunge ambayo yalianza jana, yangekuchukua siku 15 na yangekamilika Septemba 29.

Septemba 30 hadi Oktoba 6 Kamati ya Uandishi ilitengewa siku tano kwa ajili ya kuandika Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu.

Oktoba 9 Kamati ya Uandishi ilikuwa iwasilishe Katiba hiyo bungeni na Oktoba 10 hadi Oktoba 21 ingekuwa siku saba kwa ajili ya kupiga kura. Baada ya hapo Bunge lilijipangia kuwa baada ya upigaji kura, wajumbe wangepewa siku tano kwa ajili ya kujadili na kupitisha masharti ya mpito.

Ratiba hiyo ya Bunge pia inaoneshakuwa Oktoba 29 na 30, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu alikuwa awasilishe kwa Rais Katiba inayopendekezwa na Bunge lake.

Sababu za maafikiano Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD) Cheyo alitaja sababu saba zilizowaongoza kuafikiana mambo hayo; moja ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, inayotaka mwisho wa mchakato wa kupata Katiba mpya, uwe kura ya maoni iliyotarajiwa kufanyika Aprili 2015.

Cheyo alisema kama itabidi kura kurudiwa kwa mujibu wa sheria iliyotajwa, ilitarajiwa kufanyika hivyo Julai 2015, muda ambao Bunge la Muungano linatakiwa liwe limevunjwa kwa ajili ya kupisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.

Alisema ili Katiba mpya itumike katika uchaguzi mkuu utakaokuja, ilionekana kuwa itabidi uhai wa Bunge na Serikali uongezwe zaidi ya 2015, jambo ambalo alisema viongozi wa vyama vya siasa hawaliungi mkono jambo hilo.

Alitaja sababu ya pili ni kwamba Bunge Maalumu la Katiba kwa sasa linafanya kazi kwa mujibu wa tangazo la Serikali namba 254 lililotolewa na Rais Kikwete Agosti mosi mwaka huu.

Tangazo hilo litatumika hadi Oktoba 4, mwaka huu ambapo Katiba inayopendekezwa ilitarajiwa kupatikana.

Alisema wajumbe walikubaliana hatua hiyo iachwe iendelee hadi ifikie mwisho, kama tangazo linavyoelekeza kuwa mwisho itakuwa Oktoba 4.
Cheyo alisema pia kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, baada ya Bunge Maalumu la Katiba kumaliza kutunga Katiba, ingefuata hatua ya kura ya maoni kuthibitisha Katiba.

Alisema kwa kutambua kuwa hatua ya kura ya maoni italazimisha Uchaguzi Mkuu 2015 kuahirishwa hivyo hatua hiyo lazima iahirishwe.

Cheyo alisema sababu nyingine ni mchakato wa Katiba uendelee baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Hivyo viongozi hao wamekubaliana Katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho haraka, ili kusaidia kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa haraka iwezekanavyo.

Katika eneo hilo viongozi hao wametaka Serikali kuchukua hatua za kisheria, ili uchaguzi huo ufanyike mapema mwakani.

Vyama vilivyoshiriki kwenye mazungumzo hayo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) NCCR Mageuzi, Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP) na chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP).

Chanzo: Habari Leo