MBOWE AWEKEWA PINGAMIZI

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewekewa pingamizi la kutogombea nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajia kufanyika wiki hii kwa madai kuwa, amekosa sifa.

Pingamizi hilo limewekwa na mgombea mwingine wa nafasiya uenyekiti wa Chadema Taifa, Kansa Mbaruku, ambapo ameliwakisha kwa viongozi wachama hicho jana.

Akizungumza baada ya kuwasilisha pingamizi hilo la kumtaka Mbowe kutogembea uenyekiti, Mbarouk alisema amefikia amuzi huo kwa madai kuwa, Mbowe hana sifa za kugombea kwa mujibu wa Katiba ya Chadema.

"Katiba ya chama chetu, inamruhusu mtu kugombea nafasi moja katika vipindi viwili na baada ya muda huo kuisha, anatakiwa kugombea nafasi nyingine tofauti na hiyo. Hivyo, Mbowe ametimiza awamu mbili katika nafasi hiyo, hivyo anapoteza sifa," alisema Mbarouk.

Alisema kuwa, yeye alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora kwa vipindi viwili na alipomaliza muda huo, alitangaza kutogombea tena nafasi hiyo ya mkoa kwa kuwa katiba haimruhusu.

"Hivyo, nilitarajia Mbowe naye aache nafasi hiyo na asigombee tena ili kuiheshimu katiba ya chama chetu," alisisitiza.

Alifafanua Juni mwaka huu, baadhi ya wanachama waliandamana hadi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu hilo hilo la Katiba ambalo linaweka wazi ukomo wa vipindi viwili na aliwaambia viongozi kama wanataka kugombea, wabadili kipengele hicho vinginevyo wakigombea bila kufanya marekebisho, hatawatambua.

Sababu nyingine za kumwekea pingamizi, alisema inatokana na kuona Katiba ya Chadema ikivunjwa mara kwa mara na Mbowe, huku akiongeza tabia hiyo ya kutoheshimu katiba ilisababisha Novemba mwaka jana kubariki kuwavua madaraka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Dk. Kitila Mkumbo, jambo ambalo ni kinyume cha katiba.

Alisema katiba ya chama hicho inatamka kuwa,  kiongozi wa ngazi ya Taifa anavuliwa madaraka na mkutano mkuu na wala si watu wachache.

"Kuna mwanachama mwingine Mecky Mziray alifukuzwa chama hicho bila kupewa muda wa kujieleza, kitendo ambacho ni kinyume cha katiba ya chama chetu," alisisitiza.

Kuhusu uchaguzi huo, alisema sura ya 7 ya katiba inasema uchaguzi unatakiwa kusimamiwa na wazee wastaafu wa chama, lakini hana uhakika hadi sasa kama yapo hayo mazingira ya kuwepo wazee hao.

Pamoja na hayo, Chadema leo itakutana na waandishi wa habari ili kuzungumzia uchaguzi huo ngazi ya Taifa. Hiyo ni kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Benson Kigaila.