Shahidi huyo mwenye umri wa miaka 17 (jina limehifadhiwa) ambaye pia ni shemeji wa Mbasha, alidai mbele ya Hakimu Wilberforce Luhwago kuwa Mei 23 mwaka huu, Mbasha alimbaka kwa mara ya kwanza wakati mkewe Flora akiwa hayupo.
Alidai siku hiyo, Flora na mumewe walitoka kwenda kufuatilia CD za video zao za nyimbo huku mtoto wao (jina tunalo) akiwa shuleni.
Alidai alishangaa kuona ghafla Mbasha alirudi nyumbani peke yake na kumlazimisha kufanya mapenzi kisha alimtukana na kumtishia kumdhuru endapo atatoa siri.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, shahidi huyo aliendelea kudai kwamba Mei 25 mwaka huu, siku ya Jumapili walikwenda kanisani na waliporudi Mbasha alilalamika kuwa ana njaa hivyo alimpa fedha kununua chipsi.
Alidai baada ya kula, Mbasha alimwambia waondoke nyumbani kwenda kumtafuta Flora ambaye hakuwepo nyumbani siku hiyo.
"Tulipanda gari aina ya Toyota Ipsum, wakati tupo njiani aliniambia nikae kiti cha mbele pamoja naye kwani nilikuwa nimekaa kiti cha nyuma. Nilikubali kukaa katika kiti hicho ndipo aliniambia kuwa ananipenda hivyo tufanye mapenzi kwani nimeshazoea," alidai shahidi.
Aliendelea kuieleza mahakama kuwa baada ya kukubali kukaa katika kiti cha mbele, Mbasha alipandisha vioo vya gari na kulaza kiti alichokuwa amekalia mtoto huyo na kuanza kumvua sketi yake na nguo za ndani.
Pamoja na hayo alimkaba shingo na kumziba mdomo kwa khanga ili asipige kelele na kumbaka kwa mara nyingine.
Shahidi huyo alieleza kwamba baada ya kitendo hicho kuisha, Mbasha alishuka kwenye gari na kumuacha dada huyo akiwa ndani ya gari na aliporudi alimtaka waendelee kufanya mapenzi kitendo ambacho mtoto huyo alikataa.
Hata hivyo, alidai baadaye alimtafuta Flora kwa simu na alipopokea hakumwambia kilichotokea hadi alipofika Sinza kwa dada zake ambako walimweleza Flora kwa njia ya simu kitendo alichofanyiwa na mumewe, huku akiwa haamini kilichotokea.
Alidai walitoka pamoja na dada zake kwenda kuripoti katika kituo cha Polisi cha Sinza na polisi waliokuwepo kituoni hapo waliwaamuru kutoa taarifa hizo katika kituo cha polisi ambacho tukio la ubakaji limetokea.
Hivyo walirudi hadi kituo cha Polisicha Tabata na kutoa taarifa.
Kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kifungu cha 186, kifungu kidogo cha tatu cha sheria za mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kinaeleza kuwa mashauri yote ya ubakaji yanatakiwa kusikilizwa katika mahakama ya siri.
Wakili Katuga aliiomba mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo katika mahakama ya siri kwa kuwa mtoto huyo yupo chini ya miaka 18 na hairuhusiwi mtu yeyote asiyehusika kusikiliza mashauri hayo.
Kesi imeahirishwa hadi Septemba 12 mwaka huu.
Mbasha anashitakiwa kwa mashitaka mawili ambayo Mei 23 mwaka huu, maeneo ya Tabata Kimanga Wilaya ya Ilala, alimbaka mtoto wa miaka 17 nyumbani kwake. Pia alidaiwa Mei 25 mwaka huu, alimbaka tena mtoto huyo ndani ya gari kinyume na sheria.