RAILA ODINGA ACHARAZWA BAKORA

Hali ya taharuki iliibuka katika mkutano wa hadhara katika jimbo la Kwale nchini Kenya, baadaya mwanamume mmoja kwenda ukumbini na kuanza kutandika bakora kiongozi wa upinzani Raila Odinga pamoja na wanasiasa wengine.

Raila alikuwa amejiunga na kikundi cha wanawake waliokuwa wanacheza densi ya kitamaduni kuwatumbuiza wageni, pamoja na gavana wa jimbo la Kwale Pwani ya Kenya Salim Mvuruya katika mkutanmo wa kisiasa.

Walikuwa wameambatana na viongozi wengine, wakiwemo, Seneta Juma Boy, Hassan Omar, Agnes Zani, James Orengo, Johnstone Muthama na wengineo.

Mwanamume huyo alimshambulia Odinga ambaye ni waziri mkuu wazamani na kumchapa mara mbili kabla ya kumgeukia gavana wa jimbo hilo na pia kumchapa mara mbili.

Hata hivyo mwanamume huyo alishindwa nguvu na walinzi wa Raila Odinga.

Polisi walithibitisha kuwa walimkamata mwanamume huyo na kumwachilia baada ya kugundua kuwa alikuwa na matatizo ya kiakili.

Haijulikani kwa nini mwanammume huyo alimshambulia Raila ila baadhi wanasema ni kwa sababu alighadhabishwa pale waziri mkuu alipocheza densi na mwanamke aliyesemekana kuwa mke wake ambaye alikuwa katika kikundi cha wanawake waliokuwa wanawatumbuiza wageni waheshimiwa.

Viongozi waliofika walilazimika kusitisha densi hiyo kabla ya mwanamume huyo kushindwa nguvu.