WANANCHI MPANDA WAGOMA KUPANDA BUS

KITUO Kikuu cha Mabasi mjini Mpanda, mkoani Katavi kilikumbwa na tafrani jana baada ya abiria kugoma kusafiri na mabasi mawili baada ya kubaini matairi yake yamechakaa.

Abiria hao waligomea kusafiri kwa mabasi ya abiria mali ya Kampuni ya AM Drama, yenye namba za usajili T740 AQD na T 468 AGC na kushinikiza warudishiwe fedha zao za nauli.

Kamanda wa Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani mkoa wa Katavi , Joseph Shilinde alilazimika kuingilia kati sakata hilo kwa kuagiza magari hayo mawili kusitisha safari zake hadi hapo yatakapowekewa tairi mpya.

Pia, aliagiza mmiliki wa mabasi hayo, kurejesha fedha za nauli zilizotolewa na abiria hao watafute usafiri mwingine.

Mabasi hayo yalikuwa yafanye safari kutoka mjini Mpanda mkoani Katavi kwenda Tabora kupitia mjini Inyonga Wilaya ya Mlele.

"Matairi ya magari haya yamechakaa, hayafai, ni vipara vitupu hatuko tayari kusafiri nayo…ukizingatia kuwa hayawezi kamwe kumudu kusafiri katika barabara za vumbi. Kutoka hapa hadi Tabora barabara ni ya vumbi ," alisema John Kikwala.