MADARAKA NYERERE AWATETEA WANAOTAKA URAIS

MTOTO wa baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Madaraka Nyerere, amesema ni hatari kwa vyama vya siasa kuwazuia watu wenye nia ya kutaka kugombea urais mwaka 2015.

Amesema kitendo cha kuwazuia ni kuwanyima nafasi wananchi kupima uwezo, uadilifu na busara zao kama wanafaa kuongoza Taifa la Tanzania.

Akizungumza juzi, mjini Butiama alipotembelewa na viongozi wa Chama cha Siasa cha ACT-Tanzania, walipofika nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, Madaraka alisema nimuhimu wa watu wanaotaka kuwania urais kujulikana mapema, huku akisisitiza kuwanyima nafasi ya kujitangaza sasa ni kuwanyima uhuru Watanzania wa kuwachambua na kuwatathmini.

"Miezi mitatu ya kuwafanya wananchi wamsikilize mtu atakayekabidhiwa madaraka ya nchi ni michache kwa ajili ya kumfanyia tathmini na kwamba, marufuku ya aina hiyo ndani ya vyama ingeachwa," alisema Madaraka.

Aliongeza, si sawa kwa viongozi wanaotaka kushika nafasi ya Urais wakakatazwa kujitangaza mapema.

Kuhusu upinzani, Madaraka alisema wanapaswa kujitofautisha na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Akizungumzia vyama kuungana ili kuiondoa CCM madarakani, alisema wakifanya hivyo wanaweza kufanikiwa, lakini alitahadharisha madhara yanayoweza kujitokeza.

Pia, alisema vyama hivyo vinatakiwa kuwa na malengo kwani bila hivyo, watakuwa wakiishia kwenye malumbano na tofauti ambazo hazitakuwa na tija kwao upinzani.

Pamoja na hayo, ACT-Tanzania walimwambia Madaraka kuwa, lengo la kufika nyumbani kwa Baba wa Taifa, ni kupata baraka zake na kujifunza maisha aliyoishi Mwalimu Nyerere, kabla na baada ya uongozi wake.

Mwenyekiti wa chama hicho, Kadawi Limbu alisema ni vema kujifunza historia ya Nyerere kwa viongozi wa Tanzania, kwa kuwa kiongozi huyo aliwaunganisha Watanzania wote.