WABUNGE WATISHIWA, WAAMBIWA WATAJUTA

JESHI la Polisi mkoani Dodoma linawasaka watu wanaosambaza vipeperushi vya vitisho dhidi ya Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba, watakaoingia bungeni leo ambapo pia watu hao walichora ukuta wa Jengo la Makao Makuu Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Vipeperushi hivyo ambavyo vimesambazwa katika maeneo mengi ya mji, ikiwemo CCM Makao Makuu, maeneo ya Bunge na Uwanja wa Jamhuri, vilikuwa vikisomeka , 'Onyo – Dodoma si mahali pa kufuja wezi wa fedha za umma, utakayeingia bungeni kuanzia kesho (leo), yatakayokupata utajuta.

"Pia, katika Jengo la CCM makao makuu na kwenye ukuta wa Uwanja wa Jamhuri, kuliandikwa maneno kwa rangi nyekundu yaliyokuwa yakisomeka `No Katiba Ufisadi'.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema jana alfajiri viliokotwa vipeperushi maeneo mbalimbali mjini Dodoma vyenye ujumbe wa kutishia kuvunjika kwa amani.

Alisema wanaendelea kupokea taarifa za watu wanaodaiwa kuandaa vipeperushi hivyo na wanafanyia kazi ili waweze kuwakamata na kushtakiwa, kulingana na kosa walilolitenda hasa la kutoa vitisho na kuhamasisha uvunjifu wa amani.

"Kila mmoja ajiepushe kujiingiza kwenye kuhamasisha uvunjifu wa amani, kujiingiza katika mikusanyiko isiyo halali na maandamano ambayo yameshapigwa marufuku na Jeshi la Polisi. Atakayekiuka na kujiingiza katika vitendo hivyo vya kiuhalifu atashurutishwa kwa nguvu zote kwa mujibu wa sheria za Nchi na kwa mamlaka iliyopewa Jeshi la Polisi," alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Dunga Omary alisema ni jambo la ajabu kuona kuwa jengo la CCM linaandikwa maneno kama yale wakati Katiba ni ya Watanzania wote.

"Kwa nini CCM wamelengwa kwani Katiba ni ya watanzania hatupaswi kulaumiwa kwa sababu ya Katiba," alisema na kuongeza kuwa, ushahidi wa mazingira ya kawaida utaona kuwa wale walioshindwa kuandamana wameamua kufanya hivyo na huko ni kufilisika kisiasa.

Kuvamia Polisi Mkoani Mwanza, uongozi wa chama hicho umesema utahakikisha watu wao waliokamatwa na jeshi la polisi, wanatolewa bila masharti, la sivyo watahamasisha wananchi kuvamia kituoni.

Hayo yalielezwa jana na Katibu wa Chadema mkoani humo, John Nzwalile wakati akizungumzia kujipanga kwao kufanya maandamano nchi nzima.

Alisema maandamano na migomo isiyo na ukomo itaendelea kufanyika ili waweze kufikisha ujumbe wao na kuongeza kuwa, watatumia akili na kudai kuwa maandamano yao yamefanikiwa kwani polisi wameandamana zaidi yao.

Tangu jana asubuhi askari polisi wamekuwa wakionekana katika maeneo mbalimbali na jiji la Mwanza ili kukabiliana na wafuasi wa chama hicho ambao wangeandama katika maeneo mbalimbali na kuishia kwa mkuu wa mkoa.

Hata hivyo, hakukuwa na maandamano huku kwenye lango kuu la kuingia katika ofisi ya mkuu wa mkoa ulinzi ukiwa umeimarishwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana aliliambia gazeti hili kuwa hadi jana majira ya saa 5.30, hakukuwa na kiongozi yeyote wa Chadema aliyekuwa anashikiliwa na jeshi hilo.


Chanzo:Habari lem