NDEGE YAANGUKA SERENGETI

UCHUNGUZI wa awali kuhusu kupotea kwa ndege ya mizigo ya Shirika la Safari Express ya nchini Kenya, umeonesha kuwa ndege hiyo yenye usajili namba 5Y SXP, aina ya Fokker 27, imepata ajali.

Taarifa ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), iliyotumwa jana jioni katika vyombo vya habari, imeonesha kuwa ndege hiyo iliyopoteza mawasiliano juzi usiku, imeonekana ikiwa imeanguka katika eneo la Kongetende Serengeti mkoani Mara.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, haijathibitika kama watu watatu ambao ni wafanyakazi waliokuwa kwenye ndege hiyo, wamepoteza maisha au la.Awali, Meneja wa Usalama na Usafiri wa Anga wa TCAA, mkoani Mwanza, John Shushu alisema, ndege hiyo iliondoka kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Mwanza Agosti 31, saa 1.26 usiku.

Mawasiliano ya mwisho na ndege hiyo, inayomilikiwa na Kampuni ya Safari Express ya Nairobi Kenya, yalikuwa saa 2:05 usiku wakati ndege ipo umbali wa kilometa 40 kutoka mpaka wa Tanzania na Kenya, ambapo ndege hiyo ilikuwa angani futi 17,000 juu ya usawa wa bahari.

Ndege ilipaswa kuvuka eneo la mpaka wa Tanzania na Kenya saa 2:11 usiku, lakini ilipoteza mawasiliano na Kituo Kikuu cha Kuongozea Ndege cha Dar es Salaam na rubani wa ndege hiyo, hakutoa taarifa kuonesha iwapo ndege yake ilikuwa na tatizo.

Baada ya kubainika kwa mabaki ya ndege hiyo, uchunguzi wa ajali hiyosasa umeanza ili kubaini sababu ya ajali hiyo. Uchunguzi huo unashirikisha wataalamu kutoka Mamlaka na Kitengo cha Uchunguzi wa Ajali.