MREMA AMSHITAKI MBATIA KWA RAIS KIKWETE

KATIKA hali ya kutapatapa kisiasa, Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), amemshtaki kwa Rais Jakaya Kikwete, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), akitaka ang'olewe ubunge.

Mrema, alitoa kituko hicho juzi mjini hapa, wakati Rais Kikwete alipokutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge kujadiliana kuhusu maridhiano ya mchakato wa katiba mpya.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, Mrema alimwomba Rais Kikwete awaonye Mbatia na John Mrema wa CHADEMA, akidai wanamsumbua jimboni wakitaka kumng'oa katika uchaguzi ujao.

Itakumbukwa kuwa Mbatia ndiye alikuwa mbunge wa kwanza kuongoza jimbo hilo mwaka 1995 katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi na John Mrema aligombea mwaka 2010 akashindwa na Mrema.

Inaelezwa kuwa, katika hali ya kuchekesha, Mrema aliacha hoja ya msingi iliyowapeleka kwa Rais na kutumbukiza malalamiko yake binafsi, akidai Mbatia ni mtu hatari kisiasa na anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa kuwa ameanza kampeni kabla ya wakati.Chanzo hicho, kiliongeza kuwa Mrema alisema pamoja na kwamba Mbatia anafanya kampeni kabla ya wakati, lakini anamlaumu zaidi Rais Kikwete kwa sababu ndiye amempa jeuri baada ya kumteua kuwa mbunge.

"Alipokuwa akisema hayo, Rais alicheka kweli kweli maana ilikuwa kama Sinema,kwa sababu alikuwa akizungumza kwa msisitizo akionyesha kukerwa na Mbatia zaidi," kilisema chanzo hicho.

Kwamba, Rais Kikwete katika kumpooza, alimtaka Mrema asiwe na wasiwasi kwa sababu wananchi wa Vunjo wanamjua mbunge wao ni nani kati yake na Mbatia.

"Rais alimuuliza kuwa kama akimwondoa Mbatia halafu akaja mwingine akamteua tena itakuwaje, lakini Mrema alishinikiza akitaka amwondoe tu na kusisitiza kwamba asipomtoa atakuwa hamtendei haki," alisema mtoa taarifa.

Mbatia alikiri kushutumiwa na Mrema mbele ya Rais na kusema kuwa hiyo ni mara ya pili kufanya hivyo hadharani."

Ni kweli alilalamika kwa Kikwete, na hii si mara yake ya kwanza kwani hata Agosti 2 mwaka huu, alinilalamikia katika kikao cha TCD.

"Namheshimu sana Mrema, ila namuomba aendelee kuwatumikia wananchi wa Vunjo lakini kwa kuwa anazidi kunifuatafuata, Septemba 6 mwaka huu, nitahutubia mkutano wa hadhara huko Vunjo kueleza msimamo wangu," alisema Mbatia.

Naye Mrema, alisema alilazimika kumfikishia kilio chake Rais Kikwete kwa sababu ndiye alimteua Mbatia."

Mbati ni mtu hatari sana, yaani anakwenda jimboni na kuwaambia wananchi mimi ni mzee na kibaya zaidi anasema tumekubaliana nimwachie jimbo.

"Nilimsema kwa Rais kwa sababu ananifanyia rafu kule jimboni, ni hatari sana," alisema Mrema.

Hivi karibuni, Mbatia alitangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo hilo huku John Mrema wa CHADEMA naye akiamini kwamba uchaguzi ujao atashinda kiti hicho.