POLISI WA DORIA WAPIGWA BOMU

SIKU chache baada ya majambazi kuvamia Kituo Kikuu cha Polisi wilayani Bukombe mkoani Geita, kuua askari wawili na kuiba silaha za moto, watu wasiofahamika wamewajeruhi askari watatu waliokuwa doria kwa kuwarushia kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu.

Askari hao kwa sasa wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea wakitibiwa majeraha.

Tukio hilo limeripotiwa kutokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa moja na nusu jioni katika kata ya Msufini karibu na daraja la Matarawe, wilayani Songea.

Mkurugenzi wa Upepelezi na Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu amethibitisha kwa njia ya simu kutokea kwa tukio hilo, ingawa alishindwa kuingia kwa undani akisema alikuwa njiani kwenda eneo la tukio akitokea mkoani Mbeya.

Hata hivyo, gazeti hili limeweza kubaini waliojeruhiwa kuwa ni WP. 10399 PC Felista aliyejeruhiwa mguu wa kulia kwenye unyayo na pajani, G 7351 PC Ramadhani aliyejeruhiwa mguu wa kulia karibu na goti na tumboni upande wa kulia na G. 5515 PC John aliyepata majeraha katika mguu wakulia chini ya goti na jeraha dogo tumboni.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Daniel Malekela, akizungumzia tuki hilo alikiri kupokea majeruhi na kueleza kuwa ametoa vipande vya bati na misumari katika majeraha ya askari hao na mpaka sasa wanaendelea na matibabu.

Habari zaidi zinasema jeshi la polisi mkoani humo kwa kushirikiana na maofisa wengine kutoka makao makuu ya jeshi, wanaendelea na uchunguzi ikiwa nipamoja na kujua chanzo cha tukio hilo.

Bomu hilo la kutupwa kwa mkono inasadikiwa limetengenezwa kienyeji.

Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu ameelezea kusikitishwa na kitendo hicho cha wahalifu kujeruhi askari kwa makusudi na amesema Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi nausalama itahakikisha wanawasaka na kuwakamata.


Chanzo: Habari leo