SHEKH PONDA AOMBA KESI ISIMAMISHWE

Wakili Nassoro Juma anayemtetea Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda ameiomba Mahakama Kuu itumie busara kusimamisha kesi ya jinai inayomkabili mteja wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.

Ponda kupitia wakili huyo, aliwasilisha maombi akitaka mahakama iamuru kesi hiyo inayomkabili mkoani Morogoro isimame ili kusubiri kwanza uamuziwa rufaa yake aliyokata mahakamani hapo.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Ponda anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi katika maeneo mbalimbali mkoani humo,likiwamo la kukaidi amri ya Mahakama ya Kisutu.

Mahakama ya Kisutu katika hukumu yake Mei 9, 2013, ilimtaka Sheikh Ponda awe mhubiri amani katika jamii likiwa ni sharti la kifungo cha mwaka mmoja nje baada ya kumtia hatiani katika kesi ya jinai mwaka 2012.

Katika kesi hiyo, Ponda na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtakaya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh59.6 milioni na kuingia kijinai kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali eneo la ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd na uchochezi.

Hata hivyo, Sheikh Ponda kupitia kwa mawakili wake alikata rufaa Mahakama Kuu kupinga hukumu.

Kutokana na rufaa hiyo, ndipo walipowasilisha maombi ya kusimamisha kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.

Jaji Lawrence Kaduri anayesikiliza maombi hayo alikubaliana na maombi ya Jamhuri na kuahirisha shauri hilo hadi Septemba 10.