UAMSHO WAOMBA MSAADA KWA RAIS

Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed amemuomba Rais kuunda tume itakayowahusisha watu kutoka Tanzania Bara, Zanzibar, wanasheria na madaktari ili waweze kuchunguza afya zao.

Sheikh Farid aliyaeleza hayo jana muda mfupi baada ya mawakili wa Serikali Peter Njike na George Barasa kuiomba mahakama kubadilisha hati ya mashtaka ya ugaidi iliyokuwa ikiwakabili na kumuunganisha Sheikh Mselem Ali Mselem na mwenzake Abdallah Said Ali na kufanya idadi ya washtakiwa hao wa ugaidi kufikia 22.

Farid alimueleza hakimu kuwa anacho cha kusema na akapewa nafasi, kisha akadai kuwa Agosti 6 na 21, 2014 walifika mahakamani hapo na kueleza matatizo, madhila na unyama waliofanyiwa na polisi na siyo magereza.

Alidai kuwa gerezani wanaishi vizuri kwa kufuata sheria isipokuwasuala la matibabu ambapo aliongeza kuwa uwezo wa bajeti yake ni mdogo hivyo wanashindwa kuwatibia jambo ambalo linasababisha waagize dawa nje wakati ugonjwa huwa hausubiri.

"Watu wameingia gerezani wanaumwa wanavuja hadi usaa kutokana na kipigo walichopewa na polisi hivyo tunamuomba Rais aunde tume kutufanyia uchunguzi wa afya zetu,"

Alisema na kuongeza;"Sisi tunachodai siyo uchochezi ninayoeleza polisi wapo wameyasikia tumekamatwa na kushtakiwa Tanganyika kwani Zanzibar siyo nchi."

Hakimu Hellen Liwa alimueleza kuwa yeye anachojua wote ni Watanzania na suala la Muungano wengine wanauamini na wengine wanataka ukazikwe Butiama.

Hakimu alimtaka aandike kwa maandishi malalamiko yake ili waweze kuyapeleka sehemu husikana kuiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 17, 2014.

Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, Hakimu Hellen Liwa alikubaliana naombi hilo na mawakili hao waliwaunganisha washtakiwa hao na kuwasomea mashtaka manne mapya.

Mawakili wa Serikali, Njike na Barasa jana walidai mbele ya Hakimu Liwa kuwa washtakiwa hao walijihusisha na mashtaka yakiwamo ya kula njama na kuwaingiza watu kushiriki vitendo vya ugaidi kinyume na kifungu cha 27(c) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi yamwaka 2002.

Njike alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja waliwaingiza nchini Sadick Absaloum na Farah Omary ili kutenda makosa ya ugaidi.

Sheikh Farid na Mselem kwa makusudi wanadaiwa kutoa msaadakwa Absaloum na Omary ili waweze kushiriki katika vitendo vya kigaidi.