POLISI, WABUNGE WAMSHUTUMU MBOWE

KAULI ya Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe ya kuagiza yafanyike maandamano na migomo nchi nzima bila kikomo, ikiwezekana hata bila ya kibali cha Polisi, imelichefua Jeshi la Polisi.
Jeshi hilo limeonya kuwa halitasita kumchukulia hatua kali, kwa kuwa anavuka mipaka ya kisiasa na kugeukia makosa ya jinai.

Aidha, limemtaka kuacha mara moja kuihamasisha jamii, kutofuata sheria na taratibu za nchi, kwani nao atakuwa anawaingiza matatani. Kauli hiyo yaJeshi la Polisi ilitolewa jana na Kamishna wa Jeshi hilo anayeshughulikia Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya jeshi hilo, jijini Dar es Salaam.

Alisema endapo Mbowe na wafuasiwake, watafanya migomo na maandamano bila ya kufuata sheria, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake, kwa kuwa tayari alishapewa onyo mara ya kwanza kufuatia kauli hiyo.

Alisema Mbowe anatakiwa kufuata taratibu na sheria kuhusu kufanya maandamano, kwani taratibu zote zipo, hivyo kwa kauli zake hizo, anavunja sheria na kuvuka mipaka iliyowekwa kugeuka kuwa jinai na siyo siasa.

''Kauli iliyotolewa na Mbowe Septemba 14 (juzi) inaashiria uvunjifu wa amani na inahamasisha jamii kutotii sheria na taratibu za nchi. Tunaonya kwamba Mbowe anatakiwa kufuta kauli yake na kwamba taratibu zote zilizowekwa zifuatwe,'' alisema Chagonja.

Awali, alisema kwamba siasa zina mipaka yake, hivyo mtu atakayetumia mwavuli wa siasa kutaka kuvuruga amani na utulivu uliopo, jeshi hilo halitamvumilia na halitasita kumchukulia hatua kali kama mhalifu mwingine.

''Masuala ya Bunge yana sheria na taratibu zake, hivyo kuna masuala mengine ya ndani ambayo hayatakiwi kutolewa nje bila ya kufuata taratibu zilizowekwa na bunge hilo, haikumpasa kusema kwamba atashinikiza wafuasi wake na wananchi kufanya maandamano yasiyofuata sheria,'' aliongeza.

Aidha, aliwaonya wananchi wote kuzingatia sheria na taratibu zote zilizowekwa katika kutekeleza jambo lolote, pia kuepuka kauli zitakazowashawishi kuvunja sheria hizo.

Alisisitiza kuwa ili kuimarisha amani na utulivu uliopo, wananchi wanatakiwa kutoshiriki katika masuala ya uvunjifu wa amani kwa namna yoyote, badala yake kushiriki katika shughuli zao za kulijenga taifa na kuleta maendeleo.

Wabunge wacharuka Wakati Jeshi la Polisi likionya kuhusu kauli zinazotajwa kuwa za kichochezi za Mbowe, Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba nao jana waliibuka na kulishutumu kundi la wajumbe wa bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa kuhamasisha watu kuandamana barabarani, kupinga kuwepo kwa Bunge hilo huku viongozi wa kundi hilo wakionesha kuwa mstari wa mbele.

Wajumbe hao pia wameshutumu kitendo cha Ukawa, kumwandama Mwenyekiti wa Bunge hilo, SamuelSitta kwa kufafanua kwamba Bungehilo, sio mali ya Sitta, bali linafanyika kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba naye ameshutumiwa kuwandiye chanzo cha vurugu na chokochoko, zinazoendelea kufanywa na UKAWA, kutokana na kauli zake, ambazo amekuwa akizitoa kuwa Bunge hilo limepoteza uhalali wa kisiasa.

Akizungumza wakati wa majadiliano bungeni, George Simbachawene alisema Ukawa wamekuwa wanafanya upotoshaji mkubwa kwa kuutangazia umma kuwa uwepo wa bunge hilo sio halali. Alionya kuwa wananchi sasa wanapaswa kupima uzalendo wa viongozi wa kundi hilo kupitia kaulizao.

Alisema Bunge hilo, sio mali ya Sitta ambaye ni Mwenyekiti na kuwa kiongozi huyo na hata Rais, hana mamlaka ya kulisitisha, kwani linaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema kwa wingi wa wajumbe walioko bungeni, hawawezi kuwa wendawazimu kuendelea na jambo ambalo sio halali.

Alisema kuwa wale ambao waliamua kutoka nje ya Bunge hilo, ndio ambao wamevunja sheria.
Simbachawene alisisitiza kuwa wanachofanya wajumbe hao ni kupinga Katiba inayopendekezwa.

Alihoji; "Hivi kuingia barabarani kuandamana ndio kutunga Katiba ya wananchi? Halafu hao Ukawa ndio wanataka tuwape nchi, kwa kweli naomba wananchi wawaone kwamba watu hawa ni wabaya".

Aliwahadharisha wananchi wasiende kuandamana, badala yake wasubiri wapige kura ya kuikubali au kuikataa Katiba hiyo na sio kwenda kuandamana.

Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alikiri kuwa bunge hilo limewakosa walio nje kwa sababu waliwahitaji ili wachangie mawazo mbadala, lakini wamekosa uzalendo kwa kukataa kurejea bungeni.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya aliwashangaa Ukawa kuwachochea vijana waandamane nchi nzima wakati viongozi wao hawashiriki maandamano hayo.

Alisema Chadema na washirika wake wa Ukawa, wasiwapeleke vijana ambao ni tumaini la taifa hili kwenye maandamano, kwani kufanya hivyo ni hatari kwa maishaya vijana hao ambao ni nguvukazi ya taifa.

Kapteni John Komba, yeye katika mchango wake alitumia muda wake mwingi, kumshutumu Jaji Warioba, kuwa ndiye aliyesababisha vurugu zote zinazoendelea nchini juu ya mchakato wa Katiba.

Alisema Jaji Warioba aliheshimiwa na Rais Jakaya Kikwete na wananchi walimheshimu, ndio maana alikabidhiwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kukusanya na kuandika mabadiliko ya Katiba na wakati huo Watanzania walikuwa kimya.

Alisema yeye baada ya kumaliza kazi yake, kazi hiyo sasa ni ya Bunge Maalumu la Katiba, lakini kila kinachofanywa na bunge hilo Jaji Warioba anawakosoa na alimwomba Mwenyekiti wa Bunge hilo, atoe tamko la kumkemea mwanasheria huyo.

Komba ambaye pia ni Mbunge wa Mbinga Magharibi, alishauri Jaji Warioba akae kimya katika kipindi hiki ambacho bunge hilo linamalizia kazi yake ya kuandika katiba hiyo.

Komba pia alimshutumu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa kujigeuza kuwa Amiri Jeshi kwa kutangaza vita na kuwataka wafuasi wake waingie barabarani nchi nzima katika maandamano ambayo hayana kikomo.

"Si mlimsikia akisema 'mko tayari kwa vita?' Wakamjibu 'tuko tayari'…akaendelea, 'lakini mjue kuna risasi mko tayari' na wafuasi wake wakajibu 'ndio tuko tayari'… hivi hii ni amani gani wanayoitangaza huko nje, hii ni hatari kwa nchi," alisema Komba."

Amos Makalla, mjumbe na Mbunge wa Mvomero ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, aliungana na wajumbe wengine, kuwashambulia Ukawa bungeni. Alisema kuwa umoja wao huo, maana yake ni umoja wa katiba ya wachache na sio ya wananchi, kama wanavyojitangaza.

Alisema kama ingekuwa ni umoja wa katiba ya wananchi walio wengi,kundi hilo lingebaki ndani ili waandike na kushiriki kwenye mambo yanayogusa wananchi wao;na sio kutoka nje ya Bunge.

Alimtaka Sitta asitishike na kauli zaUkawa, badala yake awe imara ili kazi iliyobaki ya kuandika Katiba yanchi imalizike.

Mwenyekiti wa Chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa aliliambia bunge hilo kuwa wenzake hao wa upinzani, wanamsakama Sitta kwa kuwa ndiye alikuwa chaguo lao wakati wa mchakato wa kumtafuta mwenyekiti wa bunge hilo.

Alisema wakati wa mchakato wa kumchagua mwenyekiti, vyama vyote vya upinzani venye wabunge ambavyo vinaunda Ukawa, walimuunga mkono Sitta kwa mategemeo kuwa angelinda maslahi yao.

Mwanasiasa huyo ambaye mara nyingi amekuwa anatofautiana na misimamo ya Ukawa tangu bunge hilo kuanza, alisema waliamini kuwa Sitta angewaunga mkono katika hoja zao za ovyo, ambazo alidai hazina faida kwa nchi, ndio maana wanamshambulia kila kukicha.

Mohammed Misanga alimtaka Sitta asitetereke kwa kuitwa king'ang'anizi, kwani wananchi walio wengi wanaliunga mkono bunge hilo, kutokana na mambo mengi yanayojadiliwa kuwahusu wao.

"Nimeongea na wananchi kwenye jimbo langu na kule Dar es Salaam wanawashangaa hawa Ukawa, maana haya mambo tunayozungumzia hapa ni ya wananchi wenyewe," alisema Misanga ambaye pia ni Mbunge wa Singida Magharibi.

Chanzo: Habari Leo