WACHINA WA 'SAMAKI WA MAGUFULI' WADAI MELI YAO

RAIA wa China waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya kuvua samaki kinyume cha sheria, wamewasilisha barua kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, kutaka warudishiwe Meli ya Tawariq 1 na samaki waliopokewa mahakamani kama vielelezo.

Barua hiyo iliwasilishwa na kampuni ya uwakili ya M and B iliyokuwa ikiwawakilisha Wachina hao na kusaini na mshirika wa kampuni hiyo, Ibrahim Bendera.

Katika barua hiyo, raia hao wanaiomba mahakama iwarudishiemeli hiyo pamoja na tani 296.3 za samaki zenye thamani ya Sh bilioni 2.074 ambazo zilipokelewa mahakamani hapo kama vielelezo katika kesi namba 38/2009 iliyokuwa inawakabili.

Hatua hiyo inatokana na amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyotolewa na Hakimu Mfawidhi Isaya Arufani Agosti 23, mwaka huu wakati akiwaachia huru washitakiwa wawili; nahodha wa meli hiyo, Hsu Chin Tai na wakala wa meli, Zhao Hanquing.

Awali watu 35 kutoka mataifa mbalimbali walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutuna baadaye kesi hiyo ilihamishiwa katika Mahakama Kuu mbele ya JajiRazia Sheikh ambaye alipokea vielelezo hivyo.

Kesi hiyo ilihamishiwa kwa Jaji Augustino Mwarija, ambaye aliwaachia huru washitakiwa 31 na kuwahukumu Tai na Hanquing kifungo cha miaka 30 jela au kulipafaini ya Sh bilioni 22.

Hata hivyo mmoja wa washitakiwa alifariki dunia wakati kesi hiyo ikiendelea.

Washitakiwa hao walikata rufaa kupinga adhabu hiyo.

Machi 28, mwaka huu, Mahakama ya Rufani iliwaachia huru kabla ya kukamatwa tena na kufunguliwa upya mashitaka hayo.

Wakati kesi hiyo ikiendelea, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), aliwasilisha hati ya kutokuwa na niaya kuendelea kuwashitaki.

Aliwaachia huru na Mahakama kuamuru warudishiwe mali zao.

Washitakiwa walikamatwa wakati Dk John Magufuli akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, hali iliyochangia samaki waliokamatwa kuitwa wa 'Magufuli' hasa baada ya serikali kuamua kutaifisha meli na pia kugawa samaki kwa wananchi, vyuo na taasisi nyingine za umma.

Kutoka: Habari Leo