Wezi wa chuma nchini Afrika
Kusini wameiba karibu kilomita kumi za chuma kwenye njia ya reli na
kusababisha uharibifu wa thamani ya dola milioni 2.3.
Sehemu kubwa ya chuma ya reli imeibwa katika
muda wa miezi michache iliyopita. Njia hiyo ya reli hutumiwa na magari
ya moshi kutoka mjini Johannesburg kwenda mjini Nigel. Taarifa hii ni
kwa mujibu wa jarida la The Star."ni wataalamu wa kuiba hao. Hakuna dalili ya wao kukosea hata kidogo,'' asema Thumbu Mahlangu,mwanakamati ya usafiri.
Msemaji wa usafiri wa reli Mike Asefovitz anakubaliana na hilo.
''Hawa wezi sio watu wadogo. Chuma hizi huwa ni nzito na kuweza kuzing'oa unahitaji mashine kubwa.''
Chuma hizo zina thamani ya dola 120,000 katika soko la vyuma kuu kuu.
Wizi huo umesababisha mabehewa mapya 34 kuegeshwa tu katika kiwanda kwani hazina pa kutumiwa. Kiwanda hicho sasa kinahofia watu zaidi ya 700 huenda wakapoteza kazi zao.
Nchini Afrika Kusini wizi wa vyuma ni tatizo kubwa sana kiasi cha kuleta hasara ya mamilioni ya dola kwa uchumi wa nchi.