WATALII 17 WAPORWA NA MAJAMBAZI

Kundi la watu wanaoaminika ni majambazi wakiwa na bunduki wamevamia Hoteli ya kitalii ya Weruweru River Lodge iliyopo wilayani Hai na kuwapora watalii fedha na vitu vingine.

Majambazi hao walipora Sh5.4 milioni, Dola 3,200 za Marekani sawa na Sh5 milioni na Pauni za Uingereza 110 sawa na Sh300,000.


Pia walipora kamera moja yenye thamani ya Sh1.5 milioni, kamera ya video yenye thamani ya Dola 3,000 sawa na Sh4.8 milioni na kamera nyingine sita za kisasa.

Taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz zilisema watalii 17 kutoka mataifa mbalimbali waliporwa huku watalii wanne wakijeruhiwa katika tukio hilo.

"Ni kweli hilo tukio lipo na tumeanzisha msako mkali wa kuwatafuta watu hao pamoja na vitu walivyoiba na tunaomba yeyote mwenye taarifa sahihi za majambazi hao watusaidie," ma Boaz.


Tukio hilo lilitokea juzi saa 9:30 alfajiri baada ya majambazi hao kufanikiwa kuingia katika hoteli hiyo na kuwakusanya watalii wote waliokuwa wamelala na kuwaweka katika hema moja.

Baada ya kuwakusanya katika tenti hilo, majambazi walirudi katika mahema ambayo watalii hao walikuwa wamefikia na kuanza kupora kila kitu zikiwamo saa na simu za mkononi.

Wakati majambazi hao wakiendeleana uporaji, walijitokeza watalii wanne ambao walikuwa wanawahi ndege Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kutibua harakati hizo.


"Hao watalii waliokuwa wanakwenda KIA wao walikuwa wamelala vyumbani kwa hiyo walipopanda kwenye gari na lilipowashwa tu wale majambazi wakataharuki," ilidokezwa.

Chanzo kimoja katika hoteli hiyo kimedokeza kuwa, baada ya gari hilo kuwashwa, majambazi hao waliokuwa na bunduki na mapanga waliliendea gari hilo na kuvunja kioo cha gari hilo.


Baada ya kuvunja kioo hicho, majambazi hao walianza kuwapora watalii hao lakini sauti za kuvunjika kwa kioo cha gari ndiko kunakodaiwa "kuwashtua" walinzi wa hoteli hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Hai ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo, Novatus Makunga aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano ili watu hao waweze kukamatwa.