MBOWE NA SLAA HAWANA SIFA ZA KUGOMBEA TENA CHADEMA

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa hawana sifa za kugombea tena uongozi wa chama hicho kwa kuwa wanabanwa na katiba yao.


Akizungumza jana ofisini kwake baada ya kuzungumza na Mbowe, Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza alisema walipata malalamiko na kuyafanyia kazi, ikiwa ni pamoja na kupitia kumbukumbu walizonazo na kubaini kuwa kipengele cha ukomo wa uongozi kiliondolewa kinyemela katika katiba ya chama hicho.


Alisema kwa kawaida vyama vyote vinapofanya mikutano huwapelekea muhtasari, hivyo Chadema nacho kiliwapelekea kumbukumbu ya Mkutano Mkuu wamwaka 2006, lakini hakuna sehemu yoyote iliyoondoa ukomo wa uongozi.


"Hivyo, hawa tayari wana vipindi viwili, wakichaguliwa katika uchaguzi unaokuja hatutawatambua. Wakitaka wabadili katiba kwa njia halali ambayo ni ya mkutano mkuu na si vinginevyo," alisema.


Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mbowe alisema hakuwa tayari kulizungumzia, akieleza kwamba amefika kwenye ofisi hiyo ya Msajili kwa masuala mengine.

"Siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa, likifikishwa kwenye Kamati Kuu ndipo nitalielezea," alisema Mbowe.


Baadaye Ofisa wa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisemakwamba Msajili alimwita Mbowe ili kumshawishi asaidie wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) warejee katika Bunge la Katiba.


"Mwenyekiti alibainisha kuwa msimamo wa Ukawa upo wazi kwamba hawatarudi katika Bunge hilo hadi pale maoni ya wananchi yatakapoanza kujadiliwa na msimamo huo hautabadilika," alisema Makene akimkariri Mbowe.

Makene alisema baada ya kutoa msimamo huo, hakuna maongezi mengine yaliyoendelea baina ya Mbowe na Msajili.


Alipoulizwa iwapo Msajili alionyesha nia pia ya kuushawishi upande wa pili wanaotaka serikali mbili, Makene alisema hawezi kufahamu, japo kwa nafasi yake, Mutungi ana uwezo wa kufanya hivyo.


Alipoulizwa iwapo Msajili pia alizungumzia suala la ukomo wa uongozi linalodaiwa kubadilishwa kinyemela, alisema:

"Kuhusu hilo Chadema tunafuatilia kwa kina taarifa zinazozagaa zikionyesha correspondence (barua) zinazotoka kwa Msajili wa Vyama juu ya Chadema na tutakapokamilisha tutatoa taarifa."


Gazeti hili jana lilichapisha taarifa iliyonukuu barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema, ikieleza kuwa kipengele hicho katika Ibara ya 6.3.2 (C) kiliondolewa kwenye katiba bila idhini ya mkutano mkuuwa chama hicho.

Jaji Mutungi alisisitiza kuwa mkuu wa chama hicho ndiye wenye mamlaka ya kurekebisha katiba, hivyo baada ya kupitia muhtasari wa Mkutano Mkuu wa mwaka 2006 suala la kuondoa kipengele cha ukomo wa uongozi halikuonyesha kujadiliwa katika mkutano huo.


Hata hivyo, akizungumza kwa simu juzi, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kipengele hicho kiliondolewa kwa vikao vya chama ambavyo ni wilaya na mkoa.


Hoja hiyo iliwasilishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa ChademaMkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na ambaye sasa si mwanachama wa chama hicho.


Chanzo: Mwananchi