KATIBU MWENEZI CCM ATUPWA JELA MWEZI KWA KUDHARAU MAHAKAMA

ZIARA ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Taifa, Philip Mangula mkoani Kigoma, imemponza Katibu Mwenezi wa chama hicho Wilaya ya Uvinza mkoani hapa, Majaliwa Zuberi na kujikuta akitupwa jela mwezi mmoja.


Zuberi, alihukumiwa kifungo hicho na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Kata ya Nguruka, wilayani Uvinza, William Mugisa kwa kosa la kudharau mahakama.


Inaelezwa kuwa wakati mahakama ikiendelea na shughuli zake jana asubuhi, Zuberi alikuwa akifanya maandalizi ya kumpokea Mangula kwenye ukumbi wa CCM Social Hall ambao uko karibu na mahakama hiyo, kwa kupiga nyimbo za kukisifu na kukipamba chama hicho.


Kutokana na kitendo cha kupiga muziki kwa sauti ya juu, Hakimu Mugisa aliagiza akaitwe katibu huyo na kumtaka akazime nyimbo hizo kutokana na kuingilia shughuli za mahakama na kumpa dakika tano akatekeleze, lakini aliporejea ukumbini aligoma.


Kutokana na kukaidi amri hiyo, Hakimu Mugisa aliagiza askari wakamkamate na kumpandisha kizimbani na kukumbana na adhabu hiyo ya kwenda jela mwezi mmoja kutokana na kuidharau mahakama.