Madai hayo yametolewa na familia za watu hao wakati walipozungumza na waandishi wa habari Kikwajuni Welesi mjini hapa na kudai watu kadhaa wameshakamatwa na kusafirishwa kwa ndege chini ya ulinzi mkali.
Aisha Othman mkazi wa Tomondo, alisema mume wake Hassan Bakar Suleiman alikamatwa usiku wa manane akiwa amelala.
"Niliwasikia watu usiku wakiita jina la mume wangu na kumtaka atoke nje kwamba ana wageni wake, tulipochungulia dirishani tulibaini kuwa ni polisi waliokuwa na silaha,"alisema Aisha.
Anasema mume wake aligoma kutoka kwa kuhofia usalama wake, lakini alikubali baada ya kushawishiwa na jirani yake ambaye naye aligongewa mlango na polisi hao.
Aisha alisema Naibu Sheha alitumika kumshawishi mume wakeatoke nje kwa kumuhakikishia usalama wake lakini alipotoka alitiwa pingu na kuingizwa katika gari la polisi.
Swalha Hamid Hemed naye alisema mume wake, Nassor Hamad Abdallah na mke mwenzake, Salma Khamis walisema mume wao alichukuliwa usiku kwa kishindo kilichoambatana na kupigwa risasi hewani.
Mke mwengine wa Nassor Abdallah, Salma Khamis, mkazi wa Tomondo alisema askari hao walifika nyumbani kwake wakimtafuta mume ambaye hakuwapo wakati huo.
"Baada ya kumkosa, walimchukua mtoto wao Hamad Nassor na kumpeleka Makao Makuu ya Polisi Zanzibar," alisema Khamis.
Watu wengine wanaodaiwa kukamatwa ni Naasor Hamad Mpendae, Said Salum (Kwarara), Said Kassim (Kikwajuni), Hassan Bakari (41), Hussein Bakari (41) wakazi wa Tomondo, Salim Ali Salim (Kiembe Samaki), Muhamed Isihaka (Tomondo), Rashid Ali Nyange (Kibweni) na Antar Humud (Kiembesamaki).
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Yussuf Ilembo alikiri jana kukamatwa kwa watu hao.