MASHAMBULIZI YAANZA TENA GAZA

Ndege za kivita za Israel zimeshambulia maeneo matatu tafauti kwenye Ukanda wa Gaza, kwa kile jeshi la nchi hiyo linachosema ni kujibu kombora moja lililorushwa na Hamas na kuangukia kwenye mji wa pwani wa Ashkelon, kusini mwa Israel hivi leo.

Majibizano ya risasi yalisikika kati ya pande hizo mbili, licha ya kutajwa kwamba zimesitisha mapigano kwa muda kupisha siku tatu za Sikukuu ya Eid al-Fitr zilizoanza leo, baada ya kukamilika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Juhudi za kimataifa zimeongezeka kusitisha mapigano hayo ya wiki tatu kwenye Ukanda wa Gaza. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano hayo mara moja na bila ya masharti yoyote.

"Baraza la Usalama linaunga mkono kikamilifu wito wa washirika wa kimataifa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitishwa mapigano mara moja na bila masharti yoyote ili kuruhusu uwasilishwaji wa bidhaa zinazohitajika haraka kwenye kipindi hiki cha Eid al-Fitr na hata baada ya hapo," amesema Eugene-Richard Gasana, ambaye ni balozi wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa na rais wa sasa Baraza la Usalama.

Jioni ya jana, Rais Barack Obama wa Marekani alimpigia simu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kumueleza wasiwasi wake juu ya idadi kubwa ya Wapalestina waliouwa na kujeruhiwa. Tayari Wapalestina 1,030 na Waisraili 43 wameshauawa hadi sasa.