Mtuhumiwa aliyefahamika kwa jina moja la Kanu, ambaye ni mkazi wa Kigoma naye amejijeruhi vibaya kwa kujikata koromeo, alipojaribu kujichinja baada ya kubaini kuwa amemuua mpenzi wake Cecilia.
Pia, mtu huyo anadaiwa kujichoma kisu tumboni. Taarifa kutoka eneo la tukio na zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari zinaeleza kuwa mtuhumiwa huyo ni mfanyabiashara wa mpunga.
Taarifa hizo zilisema mtu huyo anatuhumiwa kutenda uhalifu huo saa mbili asubuhi nyumbani kwa shemeji wa marehemu, aitwaye Mashaka Hanja katika Mtaa wa Majengo "B" mjini hapa.
Ilidaiwa kuwa katika uhai wake, Cesilia alikuwa akiishi kwa dada yake, ambaye ni mke wa Mashaka Hanja na alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Kanu, ambaye alikuwa amepanga katika nyumba hiyo.
Mashuhuda na majirani wa Mashaka, walidai kuwa siku hiyo yatukio, Cesilia aliamka saa mbili asubuhi na kuanza kufagia uwanja wa nyumba hiyo ya shemeji yake Mashaka.
Inadaiwa kuwa wakati Cecilia akiendelea kufanya usafi katika nyumba hiyo, Kanu alitoka nje ya chumba alichopanga katika nyumba hiyo na kumwita Cesilia, kisha wote wakaingia ndani ya chumba chake.
"Tulimsikia Kanu akimwita Cecilia, kisha tukawaona wote wakingia katika chumba alichopanga Kanu, ndipo ghafla tukasikia Kanu akifokakwa sauti kubwa, akimshutumu Cesilia kuwa siku hizi amekuwa hamjali kabisa, kwa kuwa ana mahusiano na mwanamume mwingine " alidai mtoa taarifa.
Inadaiwa baada ya mabishano ya muda mfupi, wapangaji na majirani walisikia Cesilia akipiga mayowe ya kuomba msaada. Lakini, jitihada zao za kuufungua mlango wa chumba hicho cha Kanu, zilishindwa kwani ulikuwa umefungwa kwa ndani.
"Tulijaribu kumsihi Kanu afungue mlango, lakini alikaidi ndipo tukalazimika kuchungulia dirishani na kushuhudia jinsi Kanu akimshambulia Cecilia kwa kisu, akimchoma sehemu mbalimbali zamwili wake ....huku Kanu akiwa ametapakaa damu mwili mzima " anadai mmoja wa mashuhuda. Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, askari Polisi walifika eneo hilo la tukio, baada ya kutaarifiwa.
Alisema polisi walikuwa na silaha, ambapo walivunja mlango wa chumba hicho cha Kanu na kuushuhudia mwili wa marehemu ukiwa umelala kwenye dimbwi la damu sakafuni, akiwa tayari mfu.
Ilidaiwa kuwa Kanu naye alikuwa amezirai, baada ya kujijeruhi vibaya shingoni na tumboni kwa kisu, baada ya kubaini kuwa amemuua mpenzi wake.
Kwa sasa Kanu amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, mjini hapa, kwa matibabu akiwa chini ya ulinzi mkali.
Kamanda Kidavashari alidai kuwa mtuhumiwa huyo, atafikishwa mahakamani baada ya kutibiwa na kupona.
Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ili ufanyiwe uchunguzi wa kitabibu, kabla ya kukabidhiwa ndugu wa marehemu kwa maandalizi ya maziko yake.