Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, Focas Malengo, alisema tukio hilo lilitokea Julai 27,mwaka huu saa mbili asubuhi kijijini hapo ambapo alijinyonga katika shamba la jirani yake.
Kamanda huyo alisema Lukato alikuwa na ugomvi wa muda mrefuna mkewe Mary Joseph (42) aliyekuwa akimtuhumu kuwa na uhusiano wa mapenzi na mwanaume mwingine kijijini hapo.
Alisema siku ya Julai 19, mwaka huu, Lukato alirejea nyumbani kwake saa nane mchana akitokea shambani na kula chakula ambapo alimlalamikia mkewe kuwa kilikuwa kibichi.
Alisema hatua hiyo ilizua ugomvi baina ya wanandoa hao ambapo Lukato alimwambia mkewe kwamba amempikia chakula kibichi kwa kuwa alichelewa kurudi nyumbani kutoka mwanaume huyo mwenye uhusiano naye wa kimapenzi.
Kamanda Malengo alisema mke waLukato alijitahidi kujijitetea kwa mumewe kuwa hakuwa ametoka nyumbani kwake siku hiyo na kumhakikishia mumewe kuwa chakula kilikuwa kimeiva.
Inadaiwa Lukato hakukubaliana na utetezi wa mkewe na aliendelea kumshutumu na baadaye akaanza kumpiga katika ugomvi uliochukua muda mrefu hatua iliyomfanya mke wa Lukato kurudi nyumbani kwa wazazi wake kwa kuhofia usalama wa maisha yake.
"Lukato alijitahidi kufanya jitihada za mara kwa mara za kumshawishi mkewe arudi nyumbani kwake ili wakaendelee kuishi kama walivyokuwa wakiishi awali lakini mkewe alikataa kurejea, hatua iliyomfanya Lukato kujinyonga," alisema Kamanda.
Alisema mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kidaktari na tayari umekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Chanzo: Habari leo